Wawekezaji nchini wametakiwa kutumia bima ili kuhakikisha mali zao zinalindwa pale majanga yanapotokea na kusababisha hasara.
Wito huo ulitolewa jana mjini Geita wakati wa hitimisho la Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini. Msuluhishi Mkuu wa Migogoro ya Bima (TIO), Aloyce Mbunito, alisema bima ni njia salama ya kulinda mali. Alieleza kuwa ofisi yake hutatua migogoro ya bima kwa njia mbadala nje ya mahakama, kwa haraka na gharama nafuu, hatua inayomlinda mtumiaji na kujenga imani ya umma kwenye biashara ya bima.
Mtathmini Mwandamizi wa Bima wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Ziwa, Jerry Mwantuke, alisema mamlaka hiyo inasimamia sekta kwa utaratibu mzuri ili Watanzania wapate huduma bora na wakinge mali zao.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Bima ya Amana, Pius Makulilo, alisema bodi hulinda wenye amana wadogo dhidi ya kupoteza fedha zao benki au taasisi ya fedha inapofilisika, hatua inayoimarisha imani ya wananchi kwenye mfumo wa fedha. Aliongeza kuwa fedha za wafanyabiashara zilizowekwa benki nazo zinalindwa kupitia bima hiyo ya amana.

