Kampuni ya Kassano Yaleta Cherehani za Kidijitali Kuboresha Ushonaji wa Nguo

Xmation Media
By -
0


Na Suleiman Shagata – Mwanza

Kampuni ya Kassano, iliyopo Nyashana katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, imeanzisha matumizi ya cherehani za kisasa zinazotumia teknolojia ya kidijitali kwa lengo la kuboresha na kurahisisha shughuli za ushonaji wa nguo pamoja na kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kisasa unaokidhi mahitaji ya soko la dunia.

Akizungumza leo jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Eustace Kassano, alisema uamuzi wa kuleta teknolojia hiyo umetokana na hitaji la kuwajengea uwezo vijana katika matumizi ya mashine za kisasa zinazotumika kushona aina zote za nguo zinazohitajika kimataifa.

Alisema Kampuni hiyo inajihusisha na ushonaji wa nguo katika viwango vya basic, standard na premium, na imetambuliwa kwa ubora wake baada ya kushinda tuzo kwenye Maonesho ya Nane Nane mwaka huu.

Aina za Nguo Zinazozalishwa

Kwa sasa Kampuni ya Kassano inazalisha nguo mbalimbali zikiwemo:

  • Track suit

  • Kaunda suit

  • Chupi aina ya boxer

  • Majoho ya mapadre na maaskofu

  • Safari suit

  • Jeans

  • Nguo za jeshi la wanyamapori

Kassano aliongeza kuwa Kampuni hiyo hupokea wanafunzi wa mafunzo ya vitendo kutoka vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) pamoja na vyuo binafsi, sambamba na vijana kutoka jamii wanaotaka kujifunza ushonaji wa nguo ili waweze kujiajiri.

Kwa sasa Kampuni hiyo ina wafanyakazi 70, huku ikiendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mnyororo wa ajira kwa wananchi wengi.

Kupunguza Uagizaji wa Huduma Kutoka Nje

Kassano alisema kutokana na dunia kuwa kijiji kimoja, Kampuni yao ilibaini kuwepo kwa ombwe la makampuni na mashirika ya ndani kutafuta wakandarasi wa kushona nguo kutoka nje ya nchi, hali iliyosababisha wao kuamua kuleta huduma hizo nchini ili fedha zibaki ndani na kunufaisha Watanzania.

Alisisitiza kuwa Kampuni ya Kassano inaunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia sekta ya ushonaji.

“Tunaomba makampuni na taasisi zote zitupatie ukandarasi wa kutengeneza nguo zozote zinazohitajika ili fedha zibaki nchini. Kwa sasa tunazalisha mashati 2,000 kwa siku na nguo za jeshi 1,000,” alisema Kassano.

Aidha aliitaka Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kiuchumi na kiviwanda ili kusaidia ukuaji wa viwanda vya ndani.

Changamoto za Malighafi

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni hiyo, Irene Eustace, alisema Kampuni inalazimika kuagiza baadhi ya malighafi kutoka nchi za Uganda, Kenya, Dubai na China kutokana na gharama kubwa za malighafi zinazozalishwa ndani ya nchi.

Alisema bei ya nguo za pamba zinazozalishwa nchini ni kubwa ukilinganisha na polyester kutoka nje, hali inayohitaji ushirikiano wa wadau wa maendeleo ili kuwekeza kwenye teknolojia itakayosaidia kutumia malighafi za ndani kwa gharama nafuu.

Umeme na Maji, Changamoto Kuu

Msimamizi wa Kampuni hiyo, Yassin Ibrahim, alisema cherehani za kidijitali zinarahisisha kazi za kuunganisha nguo, kumalizia (finishing) na kunyosha kwa viwango vya kisasa vinavyotambulika duniani.

Aliongeza kuwa Kampuni hushona nguo kwa oda kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo:

  • Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT)

  • Kanisa Katoliki (RC)

  • Bugando Medical Center (BMC)

  • Shule mbalimbali

Hata hivyo, Ibrahim aliomba Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongeza mgawo wa umeme katika eneo hilo pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha upatikanaji wa maji bila kukatika, kwani huduma hizo ni muhimu kwa uendeshaji wa shughuli zao za kila siku.




Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default