TANGA, TANZANIA — Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameitaka Serikali kuangalia namna dawa zinazobuniwa na wagunduzi, watafiti na wabunifu wa Tanzania, baada ya kupita michakato yote ya kisayansi na maabara, zitambuliwe kama “Dawa za Tanzania” badala ya kuitwa kwa ujumla kama tiba za asili.
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wananchi katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi, Ugunduzi na Ubunifu Kitaifa, yaliyofanyika katika viwanja vya Usagara jijini Tanga.
Amesema dawa zinazobuniwa na watafiti na wabunifu nchini zinapaswa kufanyiwa vipimo na kuthibitishwa kisayansi kabla ya kupewa hadhi ya kutibu ugonjwa fulani.
«“Dawa zikishapita mchakato wote wa maabara na ikabainika inatibu ugonjwa fulani, zipewe jina la Dawa za Tanzania za kutibu magonjwa husika,” alisema Dkt. Nchemba.»
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, matumizi ya jina “Dawa za Tanzania” yanaweza kusaidia kuondoa dhana inayoweza kujengeka kwa baadhi ya watu kwamba bidhaa hizo ni tiba za jadi zinazotokana na imani au mila za mababu.
Alisema hatua hiyo inaweza pia kuongeza imani ya wananchi katika bidhaa zinazotengenezwa na wataalamu wa Tanzania, huku ikifungua fursa zaidi za dawa hizo kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Dkt. Nchemba aliwataka Watanzania kuwaamini watafiti na wagunduzi wa ndani ambao bidhaa zao zimepitia michakato ya kisayansi, maabara na taratibu zinazohitajika kabla ya kuruhusiwa kutumika.
Serikali Kusimamia Viwango vya Elimu
Katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali haina mpango wa kulegeza viwango vya elimu nchini, bali itaendelea kusimamia miongozo inayolenga kuhakikisha Tanzania inatoa elimu yenye ubora na inayokidhi viwango vya kimataifa.
Prof. Mkenda amesema mfumo wa elimu unapaswa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujiajiri, kuendelea na masomo na kuwa mbunifu badala ya kuhitimu akiwa anafikiria kuajiriwa pekee.
Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya ufundi na ujuzi ili Tanzania ipate wataalamu wa kutosha katika sekta mbalimbali, wakiwemo wanasayansi, watafiti, wagunduzi na wataalamu wa afya.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuzingatia viwango na miongozo ya taasisi husika, ikiwemo NACTVET na TCU, katika kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inalingana na viwango vya kimataifa.
Taasisi 91 Zashiriki Maadhimisho
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema jumla ya taasisi 91 zimeshiriki katika maadhimisho hayo ya mwaka huu.
Amesema taasisi hizo zimepata fursa ya kubadilishana uzoefu na kuonesha bunifu mbalimbali zinazolenga kutoa suluhisho kwa changamoto za kijamii na kiuchumi zinazolikabili Taifa.
Maadhimisho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha uwezo wa Watanzania katika elimu, ujuzi, sayansi, utafiti, ugunduzi na ubunifu, huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa kuendeleza bidhaa na teknolojia zinazozalishwa na wataalamu wa ndani.
Kauli ya Waziri Mkuu kuhusu kuitambua bidhaa za dawa zilizothibitishwa kisayansi kama “Dawa za Tanzania” imeweka msisitizo mpya katika kuongeza thamani, kuaminika na ushindani wa ubunifu wa Kitanzania katika soko la ndani na la kimataifa.






