Kampuni ya Algeria Kuwekeza Viwanda Vitatu vya Ubanguaji wa Korosho Tanzania

Xmation Media
By -
0


Na: [NEEMA KQNDORO ] | Agosti 21, 2026

Kampuni ya ubanguaji wa korosho ya Sarl Anacard’Or kutoka Algeria inatarajia kupanua uwekezaji wake nchini Tanzania kwa kujenga viwanda vitatu vya kisasa vya ubanguaji wa korosho, hatua inayolenga kuongeza thamani ya zao hilo na kunufaika zaidi na soko la dunia.

Mpango huo umeelezwa na Mmiliki na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. Walid Dib, wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, ambaye alikuwa katika ziara kwenye kiwanda cha kampuni hiyo jijini Oran, Algeria.

Kiwanda cha kwanza kujengwa Masasi

Kwa mujibu wa Bw. Dib, kiwanda cha kwanza kinatarajiwa kujengwa Masasi, mkoani Mtwara, eneo ambalo ni miongoni mwa maeneo yanayozalisha kwa wingi korosho nchini Tanzania.

Alisema kiwanda hicho kitatumia mashine za kisasa kutoka Vietnam, huku kampuni hiyo ikiwa tayari imeanza mchakato wa usajili wa kampuni itakayosimamia uwekezaji huo kwa jina la Kilimanjaro Nuts Limited, ambayo imeanzishwa kwa kushirikiana na mbia wa ndani.

“Korosho ya Tanzania ina ubora wa kipekee na tumeamua tujenge viwanda vitatu tukianzia na cha Masasi mkoani Mtwara kitakachotumia mashine za kisasa kutoka Vietnam,” alisema Bw. Dib.

Serikali yaahidi ushirikiano kwa mwekezaji



Kwa upande wake, Balozi Matinyi alimpongeza Bw. Dib kwa kuanza mchakato wa kuwekeza nchini Tanzania, akisema Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo.

Balozi huyo alisema uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza ajira kwa Watanzania, kuongeza mapato ya Serikali, kuleta ujuzi mpya pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni nchini.

“Ni nia ya serikali kuhakikisha kuwa uwekezaji wa viwanda vya ubanguaji unaongezeka nchini ili kulipa thamani zaidi zao hili kabla ya kuuzwa nje na kupunguza uuzaji wa korosho ambazo hazijabanguliwa,” alisema Balozi Matinyi.

Mashine kutoka Vietnam kuwasili nchini

Bw. Dib alieleza kuwa kampuni hiyo tayari imeanza maandalizi ya uwekezaji huo kwa kuandaa maghala ya kuhifadhia korosho wilayani Masasi, mkoani Mtwara.

Alisema kuwa mwezi Septemba 2026 kampuni hiyo inatarajia kuagiza mashine kutoka Vietnam, ambazo zinatarajiwa kuwasili Tanzania zikiwa pamoja na wataalamu watakaotoa mafunzo kwa wataalamu na wafanyakazi wa Tanzania.

Kwa mujibu wa mpango huo, mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza Januari 2027.

Kampuni ya Algeria yaongeza ununuzi wa korosho Tanzania



Akielezea mafanikio ya kampuni yake katika biashara ya korosho ya Tanzania, Bw. Dib alimwonesha Balozi Matinyi mchakato wa uzalishaji unaofanyika katika kiwanda chake jijini Oran.

Alisema korosho ya Tanzania inapitia hatua 11 za uzalishaji kabla ya kufungashwa na kuwa tayari kwa ajili ya kuuzwa katika masoko mbalimbali.

Kutokana na ubora wa korosho hiyo, Bw. Dib alisema kampuni yake imeamua kuongeza utegemezi wake kwa korosho inayozalishwa nchini Tanzania.

“Nilipokea makontena sita mwezi uliopita; sasa hivi nina mengine sita bandarini Oran huku saba yakiwa njiani baharini na mengine saba bandarini Dar es Salaam yakisubiri kuanza safari, na kila kontena limebeba tani 27 za korosho,” alisema.

Tanzania yazalisha zaidi ya tani 617,000 za korosho



Akihitimisha ziara yake katika kiwanda hicho, Balozi Matinyi alisema juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) zimechangia kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania ilizalisha jumla ya tani 617,683 za korosho katika msimu wa 2025/26, ambazo ziliingiza mapato ya takribani Shilingi trilioni 1.25.

Balozi Matinyi alisema kiwango hicho kinaifanya Tanzania kuendelea kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa korosho duniani, baada ya Côte d’Ivoire, Vietnam na India.

Uwekezaji wa kampuni ya Sarl Anacard’Or unatarajiwa kuongeza thamani ya korosho inayozalishwa nchini kwa kuhakikisha sehemu kubwa ya zao hilo inabanguliwa na kusindikwa ndani ya Tanzania kabla ya kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

Iwapo mpango wa kujenga viwanda vitatu utatekelezwa kama ulivyopangwa, hatua hiyo inaweza kuongeza ajira, kukuza shughuli za viwanda, kuongeza mapato ya wakulima na Serikali, pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika mnyororo wa thamani wa korosho duniani.

Imetolewa na: Ubalozi wa Tanzania, Algiers, Algeria — Agosti 20, 2026.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default