NCU yasambaza miche 30,000 ya kahawa Ukerewe kupambana na kudorora kwa bei ya pamba

Xmation Media
By -
0

 



NA SULEIMAN SHAGATA, MWANZA


Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU) Mkoani Mwanza kimesambaza zaidi ya miche 30,000 ya kahawa kwa wanachama wake katika Wilaya ya Ukerewe katika jitihada za kuwasaidia wakulima kupata zao mbadala kufuatia kushuka kwa bei ya pamba.


Akizungumza jijini Mwanza, Meneja wa Biashara na Masoko wa NCU, Priscilla Cosam, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto zinazolikabili zao la pamba na kuwawezesha wakulima kuendelea kuzalisha mazao yenye tija kiuchumi.



Cosam alisema maeneo ya Ukerewe na Buchosa hapo awali yalikuwa yakilima kahawa, na kutokana na hali ya hewa kuruhusu ustawi wa zao hilo, NCU imeamua kurejesha rasmi kilimo hicho kupitia sera mpya inayowapa wakulima nafasi ya kujikita katika mazao mbadala kama mpunga, dengu na choroko.


"Tumeanza kutoa elimu ya kilimo cha kahawa Buchosa na Ukerewe. Kwa sasa, wakulima wa Ukerewe wameanza rasmi kulima kutokana na mwamko mkubwa," alisema Cosam.



Alifafanua kuwa lengo la NCU ni kusambaza jumla ya miche 400,000 kwa wanachama wake, ambapo mwitikio wa wakulima kulima kahawa umeendelea kuongezeka sambamba na utoaji wa elimu.


Cosam aliongeza kuwa NCU inalenga kurejesha mahusiano mazuri na wanachama wake kwa kuimarisha huduma za ushauri, upatikanaji wa pembejeo, pamoja na kuwawezesha wakulima kiuchumi ili kuwainua kimaendeleo.



Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default