NA SULEIMAN SHAGATA, MWANZA
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza wametoa wito kwa viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha juhudi za maridhiano zinazochukuliwa kwa sasa zinazaa matokeo chanya, ili kufanikisha maelewano ya pande zinazovutana na kurejesha utengamano wa nchi.
Wito huo umetolewa leo jijini Mwanza, kufuatia matukio ya machafuko yaliyosababisha vifo, ulemavu, kupotea kwa watu na uharibifu wa mali katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa Watemi wa Usukumani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Watemi wa Mkoa wa Mwanza, Josephat Nkingwa, maarufu kama Chifu Kisendi II wa Busumabu, alisema maridhiano huwa na maana pale pande husika zinapokutana, kusikilizana na kufikia mwafaka wenye tija.
> “Hata Mzee Nelson Mandela alipotoka gerezani aliunda tume ya maridhiano ili kuzuia visasi kati ya Umkhonto we Sizwe na makaburu,” alisema Chifu Kisendi.
Alifafanua kuwa tangu enzi za mababu, pale kulipotokea migogoro na kuhitajika usuluhishi, upande uliokosea ulilipa faini na pande zote mbili kuhitimisha kwa kushikana mikono kama ishara ya kusameheana na kuanza upya.
Kwa upande mwingine, kijana mmoja ambaye hakutaka jina lake kutajwa, alisema ni muhimu kwa watawala kusikiliza sauti za wanaowatawala ili kuzuia migongano na mitafaruku kwenye jamii.
Alisema maridhiano yanapaswa kugusa maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakilalamikia ikiwemo mchakato wa katiba mpya pamoja na hatua madhubuti za kukomesha utekaji wa wananchi ambao umekuwa ukiripotiwa kutokea nchini.
> “Nashauri rasimu ya Katiba Mpya iwe ile maarufu kama ya Waryoba, kwa sababu ina majibu ya msingi kuhusu changamoto zinazojitokeza kwa sasa,” alisema.




