NA SULEIMAN SHAGATA, MWANZA
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza, imeidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 6.5 kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya matengenezo na uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Akizungumza jijini Mwanza, Meneja wa TARURA Nyamagana, Mhandisi Dunstan Kishaka, alisema kuwa tayari serikali kupitia Mfuko wa Barabara imepitisha zaidi ya shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitano ya awali.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kishaka, miradi hiyo itahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo tofauti ya jiji, ujenzi na ukarabati wa mitaro ya kupitisha maji ya mvua, pamoja na ufungaji wa taa za barabarani ili kuboresha usalama kwa watumiaji wa barabara.
Alitaja baadhi ya barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni pamoja na:
Barabara ya Shadi – urefu wa mita 200
Buhongwa – Bulale – urefu wa mita 200 kwa gharama ya shilingi milioni 385
Isamilo – Ofisi ya Mkuu wa Wilaya – urefu wa mita 200
Mwananchi – Mahina – urefu wa mita 300
Bismark – urefu wa mita 200
Hata hivyo, Mhandisi Kishaka alibainisha kuwepo kwa changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji wa miradi, ikiwemo tabia ya wananchi kutupa taka kwenye mitaro hali inayosababisha kuziba kwa mitaro na maji kutuama barabarani nyakati za mvua.
Aliongeza kuwa malalamiko kutoka kwa wananchi pia huchangia ucheleweshaji wa kazi, hasa pale marekebisho yanapogusa maeneo yao. “Kila eneo linapohitajika kufanyiwa ukarabati, malalamiko huibuka, jambo linalokwamisha kasi ya miradi,” alisema.
Mhandisi Kishaka aliwataka wananchi kuacha vitendo vya uharibifu wa miundombinu, ikiwemo kuchoma na kuvunja barabara kama ilivyoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu, akisema vitendo hivyo vinalisababishia taifa hasara kubwa.




