Naibu Waziri Munde Awataka Waandishi Kutumia Nafasi Yao Kuelimisha Umma Kuhusu Sera za Serikali

Xmation Media
By -
0

 


Na Ashton Balaigwa, Morogoro


Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), amevitaka vyombo vya habari kutumia nafasi yake ya kimkakati kuwaelimisha wananchi na wadau kuhusu sera na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali, kwa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka.


Mhandisi Munde ameyasema hayo mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025.


Amesema sera hiyo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa shughuli za mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma, kwa kuwa inaweka mwelekeo wa namna ya kupanga, kuratibu, kutekeleza na kufuatilia shughuli hizo kwa kuzingatia ufanisi, uwajibikaji, uwazi na thamani ya fedha za umma.


“Mnyororo wa ugavi unahusisha hatua mbalimbali, kuanzia uchambuzi na upangaji wa mahitaji, ununuzi, ugomboaji na usambazaji, hadi upokeaji, utunzaji, uhifadhi, matumizi na uondoshaji wa bidhaa, vifaa na mali,” alisema Mhandisi Munde.


Usimamizi wa mnyororo wa ugavi unaathiri huduma kwa wananchi


Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa usimamizi wa mnyororo wa ugavi una athari za moja kwa moja katika namna rasilimali za umma zinavyotumika na jinsi huduma zinavyowafikia wananchi.


“Usimamizi wake una athari za moja kwa moja katika namna rasilimali za umma zinavyotumika na namna huduma zinavyowafikia wananchi,” alisema.


Kwa mujibu wa Mhandisi Munde, umuhimu wa sera hiyo unapaswa kuangaliwa katika muktadha wa vipaumbele vya kitaifa, ikiwemo matumizi bora ya rasilimali za umma, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kuimarisha uwajibikaji pamoja na kutumia teknolojia katika kujenga uchumi wenye tija, ushindani, jumuishi na endelevu.


Amesema utekelezaji wa sera hiyo unapaswa kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na mipango mingine ya kitaifa inayolenga kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


Waandishi watakiwa kutoa taarifa sahihi kwa wananchi


Mhandisi Munde amesema wananchi wanahitaji kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu masuala yanayogusa maisha yao, akisisitiza kuwa jukumu hilo linawahusu waandishi wa habari moja kwa moja.


Amesema waandishi wa habari ni miongoni mwa wadau muhimu katika kutoa elimu na taarifa kwa umma, hivyo wanapaswa kuelewa sera na miongozo mbalimbali ili waweze kuifikisha kwa wananchi kwa usahihi na lugha inayoeleweka.


Mafunzo yalenga kuongeza uelewa wa sera


Awali, Kaimu Kamishna wa Sera za Ununuzi wa Umma wa Wizara ya Fedha, Alex Haraba, alisema mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma kwa kushirikiana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.


Haraba alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa wahariri na waandishi wa habari kuhusu dhana, maudhui, misingi na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025.


Alisema washiriki watawezeshwa namna ya kuchambua, kutafsiri na kuwasilisha masuala yanayohusu mnyororo wa ugavi kwa usahihi, kwa lugha inayoeleweka na kwa kuzingatia taarifa rasmi, takwimu na ushahidi.


“Sera hii ilizinduliwa rasmi tarehe 8 Aprili 2026, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma,” alisema Haraba.


Mnyororo wa ugavi si ununuzi pekee


Haraba alisema sera hiyo inautazama mnyororo wa ugavi kwa mtazamo mpana unaojumuisha hatua mbalimbali, kuanzia utambuzi na upangaji wa mahitaji, ununuzi, ugomboaji na usambazaji, hadi uondoshaji wa bidhaa, vifaa na mali.


Alisisitiza kuwa usimamizi wa mnyororo wa ugavi si suala la ununuzi pekee kama ilivyozoeleka, bali ni mfumo mpana unaojumuisha hatua mbalimbali za shughuli hizo na unaohusisha taasisi za umma pamoja na wadau wengine katika utekelezaji wake.


“Shughuli hizi zinatekelezwa kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024 pamoja na marekebisho yake,” alisema.


Aidha, Haraba alisema miongozo mbalimbali ya ununuzi wa umma na ugavi inaandaliwa na kutolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), huku utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma ukifanyika kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).


Vyombo vya habari vyasisitizwa kuongeza uelewa


Haraba alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuelimisha na kufikisha taarifa za Serikali kwa umma.


Kwa msingi huo, alisema ni muhimu kwa wahariri na waandishi wa habari kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu dhana, mifumo, taratibu na masuala mbalimbali yanayohusika katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi.


Mafunzo hayo ya siku mbili yanatarajiwa kuwawezesha wanahabari kuelewa kwa kina sera hiyo na namna ya kuwasilisha taarifa zake kwa umma kwa usahihi, kwa kuzingatia taarifa rasmi, takwimu na ushahidi.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default