PANGANI, TANGA — Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MCC), Rajabu Abdallah, ametoa Sh milioni 100 ikiwa ni sehemu ya fedha zitakazotumika katika ujenzi wa Soko Kuu katika Kata ya Mikinguni, Wilaya ya Pangani.
Fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa soko hilo, ambao unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2026/2027. Mradi huo unakadiriwa kugharimu jumla ya Sh milioni 300 na unatarajiwa kuwa na manufaa kwa wananchi pamoja na wafanyabiashara wa Kata ya Mikinguni.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Stahabu, Kata ya Mikinguni, mara baada ya kukabidhi hundi hiyo, Rajabu ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kusimamia kikamilifu ujenzi wa soko hilo ili kuhakikisha mradi huo unaleta tija kwa wananchi.
Amesema mradi huo unaweza pia kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo, hasa kutokana na ujenzi wa barabara unaoendelea kuunganisha Tanga na Bagamoyo.
Rajabu pia amewataka watendaji na wataalamu ndani ya Mkoa wa Tanga kutambua wajibu wao wa kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili.
«“Kazi ya Chama ni kusimamia Serikali kuhakikisha inatekeleza iliyoyaahidi kwenye Ilani yake. Watendaji hampaswi kukaa maofisini, tunataka mkatatue kero za wananchi. Mtaalamu yeyote anayeona Chama kinamfatafata ajue kabisa Tanga haimfai,” amesisitiza.»
Atoa Sh milioni 10 kwa wajasiriamali
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Tanga ametoa Sh milioni 10 kwa ajili ya kikundi cha wajasiriamali wa Kijiji cha Mikinguni, Wilaya ya Pangani.
Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kuongeza uwezo wa kikundi hicho katika shughuli zao za ujasiriamali na kuimarisha shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Aweso Akabidhi Mashine ya Kuchapisha Mitihani
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amekabidhi mashine kwa ajili ya kuchapisha mitihani itakayotumika katika shule ya sekondari iliyopo Kata ya Mikinguni, ambayo imepewa jina lake.
Hatua hiyo imekuja baada ya Aweso kupata taarifa kuhusu wanafunzi kuchangishwa fedha kila unapofika muda wa mitihani.
Baada ya kupata taarifa hizo, Aweso amepiga marufuku zoezi hilo na kutoa mashine hiyo ili kusaidia kutatua changamoto hiyo.
Aweso pia ameahidi kukutana na wananchi wa Wilaya ya Pangani, hususan wanawake, ili kujadili namna ya kuwawezesha kiuchumi na kuwasaidia kujikwamua kutoka kwenye mikopo yenye masharti yanayowaumiza.
«“Mmetuchagua, tumekuwa viongozi. Tumeona mnavyoumia na mikopo chechefu na kausha damu. Hivi karibuni tutakuwa tukikaa kikao cha pamoja na kuona namna gani ya kuwezeshana kiuchumi ili mpate faida ya kutuchagua sisi vijana wenu tuwatumikie,” amesema Aweso.»
Pangani yazidi kufunguka kiuchumi
Wilaya ya Pangani inaendelea kupata miradi mbalimbali inayolenga kuongeza shughuli za kiuchumi na fursa kwa wananchi.
Mbali na ujenzi wa barabara unaoendelea kutoka Tanga hadi Bagamoyo, pia kuna mipango ya kutekelezwa kwa miradi mingine ya uwekezaji, ikiwemo kiwanda cha sukari pamoja na kiwanda cha madini.
Miradi hiyo inatarajiwa kuongeza fursa za ajira, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi kwa wakazi wa Pangani na maeneo jirani.



