MOROGORO: Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Lucy Kombani, amekutana na viongozi wa wanawake wajane wa Kikundi cha Muinue Mjane cha Manispaa ya Morogoro, ambapo ametoa msaada kwa wanakikundi wapatao 60 wanaotarajia kushiriki Kongamano la Wajane Kitaifa linalofanyika mkoani Dodoma.
Mbali na msaada huo, Mheshimiwa Lucy Kombani ameahidi kugharamia mafunzo maalumu kwa wanawake hao yatakayotolewa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), kwa lengo la kuwawezesha kupata ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali na hivyo kuongeza kipato.
Akizungumza wakati wa kukutana na viongozi hao, Mheshimiwa Kombani amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wajane kujitegemea kiuchumi na kupunguza utegemezi.
Amesisitiza kuwa kuwa mjane hakumaanishi kuwa mtu anapaswa kuwa ombaomba, bali ni muhimu wajane kupata fursa, maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuendesha maisha yao na familia zao.
«“Mjane siyo lazima awe ombaomba. Wanapaswa kupambana ili kuendelea na maisha yao, kwa sababu wana jukumu pia la kutunza familia zao kama wazazi waliobaki,” alisema Mheshimiwa Lucy Kombani.»
Hatua hiyo inatarajiwa kuwasaidia wanawake hao kujenga uwezo wa kiuchumi kupitia ujuzi wa uzalishaji na ujasiriamali, huku wakitumia fursa za mafunzo kuongeza thamani ya bidhaa wanazoweza kuzalisha na kupata kipato.
Kongamano la Wajane Kitaifa linalofanyika Dodoma linatarajiwa kuwa pia fursa kwa wajane kutoka maeneo mbalimbali nchini kukutana, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto pamoja na fursa zinazoweza kuwasaidia katika maisha yao na maendeleo ya familia zao.
