Dar es Salaam. Familia za David Mushi na Mariam Mongi, zinazodai kuwa wamiliki halali wa eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 10 lililopo Madale, Mtaa wa Scout, Wilaya ya Kinondoni, zimeeleza msimamo wao kuhusu utekelezaji wa amri ya Mahakama na kukamatwa kwa baadhi ya wanafamilia. Kupitia taarifa iliyotolewa na mwanasheria wao, Wilson Ogunde, Septemba 22, 2026, familia hizo zimesema zimenunua eneo hilo mwaka 1994 na zinamiliki hati sita za umiliki zilizotolewa mwaka 2009.
Familia hiyo imesema haki yake ya umiliki imewahi kujadiliwa katika ngazi mbalimbali za Mahakama, ikiwemo Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mahakama ya Rufani Julai 2, 2022 katika Shauri Na. 286 la 2016 ilitoa uamuzi unaoiunga mkono familia hiyo, huku Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, katika Shauri Na. 316 la 2010 ikitoa uamuzi Oktoba 28, 2022 kuhusu umiliki wa eneo hilo.
Aidha, familia hiyo imesema mwaka 2023 Mahakama Kuu katika Shauri Na. 261133 la 2023, chini ya Jaji Msafiri, iliamuru irejeshwe katika eneo hilo pamoja na kulipwa fidia ya Sh milioni 80. Taarifa hiyo inaeleza kuwa hatua za utekelezaji ziliendelea hadi Mei 9, 2025, ambapo Maombi ya Ukazaji wa Hukumu Na. 11992 la 2024 yaliamriwa na Msajili Mwakatobe na dalali wa Mahakama kuteuliwa.
Kwa mujibu wa familia hiyo, kuanzia Agosti 2025 notisi za kuondoka zilianza kutolewa kwa watu waliokuwa katika eneo hilo, kabla ya zoezi la kuwaondoa kutekelezwa Septemba 3, 2026 kupitia dalali wa Mahakama chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi. Familia imekanusha taarifa kwamba watu hao waliondolewa bila taarifa, ikisema walikuwa wamepewa notisi tangu mwaka 2025.
Familia hiyo imesema wakati huo juhudi za kupata suluhu zilikuwa zikiendelea kupitia Mkuu wa Wilaya na Kamati ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Imeeleza kuwa makubaliano yalifikiwa na baadhi ya familia zilizokuwa katika eneo hilo, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa kwa wengine 12 waliokuwa wamefungua mashauri mengine mahakamani wakati mchakato wa usuluhishi ukiendelea.
Kuhusu chanzo cha mgogoro, familia hiyo imemtaja Abdallah Kitwanga, ikidai kuwa aliuza vipande vya ardhi hiyo kwa watu wengine wakati shauri likiendelea mahakamani. Pia imemtaja Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Gratian Mbelwa, ikidai kuwa alisaini nyaraka za umiliki kwa familia inayodai kuwa mmiliki halali na baadaye akasaini nyaraka nyingine kwa wanunuzi wa vipande hivyo. Familia imeomba uchunguzi ufanyike kuhusu miamala hiyo na hatua zichukuliwe kwa watakaobainika kuhusika.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuhusu ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika eneo hilo Septemba 19, 2026, ambako inadaiwa aliwasikiliza watu walioondolewa na kuagiza wanafamilia wa Mushi wakamatwe kwa kutokuwepo eneo hilo. Familia imesema haikuwa na taarifa kuhusu ziara hiyo, ikieleza kuwa siku moja kabla ilikuwa kwenye kikao cha usuluhishi kilichoongozwa na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi pamoja na wanasheria wake.
Familia hiyo imesema baada ya kupata taarifa za agizo hilo kupitia mitandao ya kijamii, wanafamilia walirejea Dar es Salaam na kujitokeza kwa hiari kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliagizwa kwenda Kituo cha Polisi Oysterbay na kuwekwa chini ya ulinzi. Waliokamatwa wanatajwa kuwa wanawake wawili wazee na vijana watatu, huku mmoja wa wanawake hao akiwa na umri wa miaka 86 na akihitaji huduma maalumu za afya.
Familia imekanusha madai ya kukaidi au kudharau mamlaka, ikisema imekuwa ikishiriki vikao mbalimbali vya Serikali, ikiwemo vya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Kamati Maalum ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mwanasheria huyo amesema familia inatambua mamlaka ya Mkuu wa Mkoa chini ya sheria, lakini inahoji mazingira ya kukamatwa kwa wanafamilia, ikidai hawakuwa eneo la tukio wakati wa ziara na baadaye walijitokeza wenyewe.
Familia za Mushi na Mongi zimeomba agizo la kukamatwa lipitiwe upya na wanafamilia waachiliwe, huku zikiitaka Serikali na vyombo vya uchunguzi, ikiwemo TAKUKURU na Jeshi la Polisi, kuchunguza madai ya uuzaji wa ardhi hiyo wakati kesi ikiendelea pamoja na uidhinishaji wa miamala. Familia hiyo imesema inaendelea kuamini katika utawala wa sheria na iko tayari kushirikiana na mamlaka katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
