Morogoro Yaweka Mkazo Kutangaza Utamaduni wa Tanzania Katika AFCON 2027

Xmation Media
By -
0

 



Na Ashton Balaigwa, Morogoro


MOROGORO: Serikali imewataka Watanzania kutumia fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kutangaza utamaduni wa makabila mbalimbali nchini, sambamba na kufanya vizuri katika mashindano hayo.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati akifungua Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linalofanyika mjini Morogoro, ambapo jumla ya washiriki 150,000 kutoka mikoa mbalimbali wanashiriki kwa kuonyesha tamaduni zao.


Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu zitakazokuwa wenyeji wa AFCON 2027, pamoja na Kenya na Uganda. Kwa upande wa Tanzania, mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika katika miji ya Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.


Akizindua tamasha hilo, Malima amesema Watanzania wanapaswa kutumia ujio wa wageni wakati wa mashindano hayo kutangaza zaidi Tanzania kupitia vivutio vya utamaduni wa makabila mbalimbali, akisisitiza kuwa utamaduni ni sehemu muhimu ya kuimarisha umoja, mshikamano na amani nchini.


Malima pia amewataka Watanzania kuendelea kuheshimu na kuthamini utamaduni wao, akieleza kuwa utamaduni ni sehemu muhimu ya kujenga heshima na utambulisho wa taifa.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema Tamasha la Kitaifa la Utamaduni lilianzishwa Mkoani Dar es Salaam, kabla ya kuhamia Songwe na Ruvuma, huku mwaka huu likifanyika Mkoani Morogoro.


Akizungumzia maandalizi ya AFCON 2027, Msigwa amewataka Watanzania kupuuza taarifa zinazodai kuwa Tanzania imeondolewa kwenye orodha ya wenyeji wa mashindano hayo.


Msigwa amesema taarifa hizo si za kweli na amesisitiza kuwa Tanzania bado ni miongoni mwa nchi zitakazokuwa wenyeji wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda.


MAELEZO YA PICHA


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, akipiga ngoma kuashiria ufunguzi wa Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linalofanyika mjini Morogoro.

Tags:

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default