DKT. KIJAJI AELEKEZA MAAFISA UHIFADHI KUHAKIKISHA MAENEO YA HIFADHI YANALINDWA NA KUHIFADHIWA

ASHRACK
By -
0


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amewaelekeza maafisa uhifadhi nchini kuhakikisha maeneo yote ya hifadhi yanalindwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Dkt. Kijaji ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma wakati wa kikao kilichowakutanisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, Wakuu wa Wilaya wa mkoa huo, watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwemo viongozi kutoka  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

 Kikao hicho kilijadili ongezeko la uvamizi na uharibifu wa misitu unaofanywa na watu mbalimbali katika maeneo ya hifadhi, hali inayohatarisha rasilimali za misitu na wanyamapori pamoja na juhudi za Serikali katika usimamizi endelevu wa maliasili.

Katika kikao hicho, Dkt. Kijaji amesisitiza kuwa maazimio yote yaliyofikiwa katika kikao hicho yanapaswa kutekelezwa kikamilifu na kwa wakati, akieleza kuwa hakuna nafasi ya uzembe katika kulinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi.

Sambamba na hilo, amewataka watendaji wote wenye dhamana ya usimamizi wa maeneo ya hifadhi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji wa hali ya juu, akionya kuwa watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Dkt. Kijaji ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuimarisha sekta ya uhifadhi kupitia utoaji wa ajira kwa wahifadhi pamoja na kuongeza bajeti ya sekta hiyo, hatua zinazochangia kuimarisha ulinzi na usimamizi wa maeneo ya hifadhi nchini.

Amesema pia ni wajibu wa viongozi wa Wizara na wa Mkoa kuhakikisha sheria zinasimamiwa kikamilifu ili kulinda rasilimali za taifa zilizopo katika maeneo ya hifadhi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, amesema kikao hicho kimekuwa na manufaa makubwa katika kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na uvamizi wa maeneo ya hifadhi na kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara na viongozi wa mkoa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Misitu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras, amesema watahakikisha maeneo yote ya misitu yanalindwa na kuhifadhiwa ipasavyo, huku akiahidi kuwa maazimio na maelekezo yote yaliyotolewa katika kikao hicho yatafanyiwa kazi kwa ufanisi.

Aidha, Dkt. Kijaji amesisitiza kuwa maelekezo yaliyotolewa na Mawaziri wanane wa kisekta kuhusu ulinzi wa maeneo ya hifadhi yatekelezwe kikamilifu katika mikoa yote nchini ili kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za taifa na kuhakikisha sheria zinafuatwa bila upendeleo.






 

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default