MWAMBA MINING Yasifu Sera ya Madini kwa Kuimarisha Amani na Ukuaji wa Sekta

Xmation Media
By -
0

MWAMBA MINING Yasifu Sera ya Madini kwa Kuimarisha Amani na Ukuaji wa Sekta


Nyarugusu – Meneja wa Mgodi wa Mwamba Mining, Habil Ezekiel, ameipongeza sera ya madini nchini kwa kusema imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya madini huku ikisaidia kupunguza migogoro na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa uchimbaji.


Akizungumza leo kufuatia mazungumzo yaliyofanyika kati ya wadau wa sekta hiyo kuhusu utaratibu wa kuiachia Mwamba Mining eneo lao walilokuwa wamewaruhusu baadhi ya wachimbaji kuendelea kufanya shughuli za uchimbaji kwa makubaliano maalum, Ezekiel alisema sheria na sera zilizopo zimeweka msingi mzuri wa usimamizi wa shughuli za madini.


Alieleza kuwa mikataba ya uchimbaji imekuwa nyenzo muhimu inayowaongoza wadau wanaofanya kazi katika maeneo yanayofanana, hivyo kusaidia kuepusha migongano na kujenga mazingira ya ushirikiano.

"Hatuna sababu ya kubugudhi au kuwanyanyasa wadau wenzetu wanaofanya shughuli za uchimbaji katika eneo hili. Tunasisitiza kila mmoja kuheshimu sheria, taratibu na makubaliano yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria za nchi," alisema Ezekiel.


Aidha, amekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye baadhi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii zinazodai kuwa wananchi waliopo katika eneo hilo wanapinga kuliachia eneo hilo Mwamba Mining.

Kwa mujibu wake, taarifa hizo si za kweli na zinalenga kupotosha umma pamoja na kujenga taswira hasi dhidi ya kampuni hiyo, huku akisisitiza kuwa mazungumzo na ushirikiano kati ya pande zote yanaendelea katika hali ya utulivu na kuheshimiana.


Mwamba Mining imeeleza itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wote wa sekta ya madini kwa kuzingatia sheria, uwazi na ushirikiano ili kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania wote.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default