CWM Yaendelea Kutetea Haki za Wafanyakazi wa Majumbani Kupitia Mafunzo kwa Makundi ya Wanawake Morogoro

Xmation Media
By -
0

Chama cha Wafanyakazi Wakatoliki (CWM) kinaendelea na jitihada zake za kutetea na kuhamasisha haki za wafanyakazi wa majumbani kwa kutoa semina na mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wanawake katika jamii.

Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa maono na misingi ya chama hicho ya kuwa sauti kwa wasio na sauti, hususan wafanyakazi wa majumbani ambao mara nyingi hukutana na changamoto na vikwazo mbalimbali wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Katika mwendelezo wa mkakati huo, Juni 5, 2026, CWM ilikutanisha wanawake Wakatoliki pamoja na makundi mengine ya wanawake katika Parokia Teule ya Mtakatifu Benedict Mkundi, Jimboni Morogoro, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutambua na kutetea haki za wafanyakazi wa majumbani.

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika mafunzo hayo ni umuhimu wa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wa majumbani, pamoja na haki na wajibu wao kama ilivyo kwa wafanyakazi wa sekta nyingine rasmi.

Akizungumza katika semina hiyo, Mratibu wa Taifa wa CWM, Edson Yeyeye, aliwataka washiriki kuendelea kuimarisha malezi ya kimaadili kwa wafanyakazi wa majumbani ili kulinda heshima, utu na maadili ya kazi hiyo muhimu katika jamii.

Kwa upande wake, Katibu wa CHODAWU Mkoa wa Morogoro, Frola Ng'eni, alisisitiza umuhimu wa wafanyakazi wa majumbani kuingizwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo NSSF, ili kuwawezesha kupata akiba na usalama wa maisha yao ya baadaye.
Aidha, alisema kuwa sekta ya wafanyakazi wa majumbani ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa familia na taifa kwa ujumla, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanapata haki zote wanazostahili bila kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji au ubaguzi.

CWM imeeleza kuwa itaendelea kuyafikia makundi mengi zaidi ya wanawake katika Jimbo la Morogoro. Katika hatua nyingine, chama hicho kinatarajia kukutana moja kwa moja na kundi la wafanyakazi wa majumbani kwa lengo la kukamilisha maandalizi ya kuwapeleka kwenye mafunzo ya ufundi stadi yatakayotolewa katika Chuo cha VETA Mikumi.

Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu muhimu ya kuwawezesha wafanyakazi wa majumbani kiuchumi na kijamii, huku ikichangia kukuza uelewa wa haki zao na kuboresha mazingira ya kazi katika sekta hiyo muhimu.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default