WAHARIRI WAIPONGEZA REA USAMBAZAJI WA GESI ASILIA LINDI, PWANI
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa pongezi kwa Serikali kupitia REA kwa mradi wa kusambaza gesi asilia unaonufaisha kaya 1,000 na shule moja — ukifadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100.
"REA imefanya kazi kubwa sana ya kufadhili mradi huu, hivyo basi mradi huu utaboresha kiwango cha maisha ya walengwa wa mradi kwa kuokoa gharama na muda wa kupika, mazingira safi afya bora na uwezeshaji wa wanawake kuongezeka."
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kusambaza miundombinu ya gesi asilia kwenye kaya takribani 1000 na shule moja ambapo mradi huo umefadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia REA.
Hayo yamezungumzwa leo Machi 8, 2026 na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw. Deodatus Balile wakati wa Ziara ya TEF Kutembelea mradi uliofadhiliwa na REA wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwenye nyumba za makazi mkoa wa Pwani.
Bw. Balile amesema kupitia mradi huo Serikali imepunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa Nishati nyingine kama mkaa wa kawaida, kuni, na mafuta ya taa na nishati gesi asilia sasa inakua ni chanzo cha nishati ya kupikia.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Mradi kutoka REA, Mha. Emmanuel Yessaya amesema kuwa Wakala ulitenga Fedha kwa ajili ya kufadhili mradi ya usambazaji wa gesi asilia kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini (REF) ambapo takribani kaya 1000 pamoja na taasisi moja zimenufaika kwa kusambaziwa miundombinu ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia majumbani katika mkoa wa Lindi na Pwani.
Kwa upande wake Mhandisi wa mradi huo kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mha. Anthony Karomba, amesema kuwa mradi huo wa kuunganisha wateja wa majumbani kwenye mtandao wa gesi asilia umegharamikiwa kwa fedha nyingi na Serikali kupitia REA na hivyo amewasihi wananchi kuendelea kuilinda miundombinu hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Kata ya Kisemvule wameishukuru Serikali kupitia REA kwa kusambaza miundombinu ya gesi asilia ya kupikia katika miji yao.
