Na SULEIMAN SHAGATA, MWANZA
WADAU wa uvuvi ndani ya Ziwa Victoria wamelezea kuwepo kwa changamoto ya kupungua kwa mazao ya samaki kwa sababu mbalimbali zinazojitokeza kwa sasa sehemu mbalimbali duniani na kuathiri uvuvi wa samaki.
Wamesema leo Jijini Mwanza katika kikao kilichowakutanisha maofisa uvuvi wa wilaya na mkoa, maofisa mazingira na usafi wa Jiji, wahadhiri wa vyuo vikuu, viongozi wa bodi ya usimamizi wa mialo (BMU) na Asasi zisizokuwa za Kiserikali (NGO) na
Wadau hao walieleza kuwa uharibifu wa mazingira, ongezeko la vifaa vya plasitiki, mitego haramu ya uvuvi na ongezeko la shughuli za uvuvi kuwa miongoni mwa sababu zinazo sababisha kupungua kwa samaki ziwani.
Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu cha Dar essalaam ambaye ni Mtafiti wa taka za plasitiki, Dk Bahati Mayoma alisema uwepo kwa matumizi ya plasitiki duniani kunasababisha madhara makubwa kwa uhai wa samaki.
Alisema bidhaa za plasitiki tani milioni 300 hadi 400 zinazozalishwa dunia kila mwaka asilimia 50 huzagaa na kusababisha tani milioni 12 kuingia majini.
"Matumizi ya vifaa vya plasitiki ni janga kwa dunia kwani katika utafiti tumekuta baadhi ya samaki kuwa na plasitiki zinazoonekana kwa macho na zisizoonekana hivyo juhudi zinahitajika kupiga marufuku ili kunusuru viumbe majini"alisema Dk Mayoma.
Dk Laison Kaganga wa Idara ya Jiografia Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza, alisema kinachotakiwa ni utashi wa maamuzi ya kisera ili kuwezesha uendelevu wa Leo na kesho kwa Ziwa Victoria.
Alisema maamuzi kama hayo yatawezesha kukomeshwa kwa madhara yote yanayosababisha kupungua kwa samaki.
Kaimu Afisa Mfawidhi Usimamizi wa Raslimali za Uvuvi Kanda ya Ziwa, Laurent Mbujilo alisema kuendelea kupungua kwa samaki kumefanya kubaki kwa viwanda vinane vya samaki kutoka 24 ndani ya Kanda ya Ziwa.
Alisema kukithiri kwa uvuvi haramu, mabadiliko ya hali ya hewa, uchafuzi wa mazingira na uvuvi wa kutumia mitego ya timba kuwa ni mojawapo ya sababu zinazopelekea kuathiri samaki ndani ya Ziwa Victoria.
Kaimu Ofisa Usafi na Mazingira Jiji la Mwanza, Oswald Mpelasoka aliwataka viongozi wa BMU kuweka utaratibu wa kuzoa uchafu na kuupeleka kwa sehemu za kutupa taka ili kuzuia kuingia majini.
Aliwataka viongozi vilevile kusimamia suala la usafi kwa kuzuia kujisadia watu, kutupa majini vinyesi ,plasitiki na vitu vingine ambavyo ni hatarishi kwa viumbe hao.
Ofisa Mazingira na Usafishaji Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene aliwataka wadau hao wa uvuvi na wananchi kuhakikisha wanakabiliana na uchafuzi wa ziwa dhidi ya bidhaa za plasitiki ili kuwezesha usalama wa mazao ya samaki ziwani ili kuwepo uendelevu.
Viongozi wa Kamati za Usimamizi wa Mialo (BMU); Thadeo Philipo Mwenyekiti BMU Igombe, Majula Masoko BMU Butuja, Charles Nyakulimba BMU Bwiru, Mwajuma Chamliho wa Mswahili na Gaspar Timbalale wa Kayenze walisema kuwa upungufu wa samaki ni mkubwa kwa sasa.
Walibainisha sababu kuwa ni utegaji kwa mitego ya timba, kutupwa kwa nyavu za plasitiki, mitego mingine haramu, uchafuzi wa ziwa na kuongezeka kwa uvuvi kwa sasa.
Wadau wameshauli elimu izidi kutolewa kwa umma juu ya jinsi ya kukabiliana na changamoto hiyo, kukomeshwa kwa matumizi ya mitego yote haramu na kuzingatiwa kwa sheria za utunzaji wa viumbe majini.




