Vijana Washauriwa Kujiajiri Badala ya Kutegemea Ajira

Xmation Media
By -
0


Na Suleiman Shagata, Mwanza


Kutokana na ongezeko la wahitimu kutoka vyuo mbalimbali nchini na upungufu wa nafasi za ajira, vijana nchini Tanzania wametakiwa kuacha kutegemea ajira pekee na badala yake wajikite katika shughuli za kujiajiri katika sekta za kilimo, ufugaji, madini na ufundi ili kuboresha maisha yao.


Wito huo umetolewa leo jijini Mwanza katika kongamano maalum lililowakutanisha vijana waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu—akiwemo shahada, stashahada, na vyuo vya kati—kwa lengo la kupeana taarifa na elimu juu ya fursa za kiuchumi zinazopatikana nchini.


Serikali: Vijana Mna nafasi Kubwa ya Kuleta Maendeleo


Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwapongeza vijana waliojitokeza na kusisitiza kuwa serikali ina wajibu wa kujenga mazingira wezeshi katika sekta za umma na binafsi.


> “Serikali inawategemea vijana katika kuleta maendeleo ya nchi. Tumeona ni vyema kuwapa taarifa ambazo hamkuwa mnazijua,” alisema Mtanda.




Aliongeza kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kuwasaidia vijana kubadilisha mtazamo kuhusu ajira, kwani kwa sasa nafasi ni chache duniani kote, hivyo ubunifu na kujiajiri ni muhimu zaidi.


Mabenki yaendelea Kutoa Fursa za Mitaji


Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Mwaloni, Cornelius Msigwa, alieleza kuwa benki hiyo ina mikopo maalum kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, kwa biashara rasmi na zisizo rasmi.


Msigwa alisema kuwa mfanyabiashara aliye na proforma invoice na akaunti ya CRDB anaweza kupata mkopo kwa ajili ya manunuzi ya biashara. Aidha, kupitia mradi wa IMBEJU, benki inatoa mikopo kwa wanawake kupitia vikundi, na kwa vijana wabunifu, CRDB kwa kushirikiana na COSTECH inaweza kutoa mkopo hadi milioni 30 kwa miradi ya ubunifu.


Sekta ya Kilimo Yaendelea Kupewa Kipaumbele


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), James Shimbe, alisema bodi hiyo inaendelea kuwawezesha wakulima kwa kuwapatia pembejeo na huduma za ugani bure ili kuboresha uzalishaji.



Alisisitiza kuwa kwa sababu ajira katika sekta binafsi na serikalini ni chache, vijana wanapaswa kutumia ubunifu wao kuwekeza kwenye sekta za kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na ufundi ili kujijenga kiuchumi.


Ushuhuda: Ufugaji Samaki Katika Vizimba Wabadilisha Maisha


Mmoja wa wanufaika wa mradi wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba, Pius Makindi, alisema kuwa alipojiunga na wenzake kuanzisha mradi huo, walipata mafanikio makubwa na sasa wameongeza idadi ya vizimba.


> “Mapato tunayopata kupitia uuzaji wa samaki yamenibadilisha kabisa. Nimeona kuwa kutegemea ajira ni kikwazo. Kujiajiri kunafungua milango mingi ya maendeleo,” alisema Makindi.



Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default