Na Suleiman Shagata, Mwanza
Baadhi ya madiwani wapya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wameomba kuandaliwa kwa semina elekezi kabla ya kuanza rasmi kutekeleza majukumu yao, ili kuwajengea uelewa wa taratibu, historia ya miradi, na mifumo ya utendaji ndani ya halmashauri.
Ombi hilo limetolewa leo wakati wa kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani jijini Mwanza, ambapo wamesema mafunzo hayo yatawawezesha kushiriki kikamilifu katika mijadala ya miradi, hususan ile ambayo ilianza kutekelezwa na awamu iliyopita lakini haijakamilika.
Diwani wa Kata ya Milongo, Nurdin Anas-Mbaji, alisema wamepokea miradi iliyokuwa ikiendelea, hivyo semina elekezi ni muhimu ili kuwajengea uwezo wa kuchangia hoja kwa ufasaha na kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa ya wananchi.
Aidha, alishauri taarifa za masuala yanayotarajiwa kujadiliwa kwenye vikao zipelekwe mapema—angalau siku saba kabla—ili madiwani wapate muda wa kusoma na kuelewa kwa kina kabla ya kikao.
Naye Diwani wa Kata ya Lwanhima, Chanila David, alisema madiwani wapya ni karibu robo tatu ya baraza zima, hivyo wengi hawana uelewa juu ya historia ya miradi ya maendeleo. Alisisitiza kuwa semina ya mwongozo ni muhimu ili kujenga msingi wa utendaji wenye tija tangu mwanzo.
“Hapa tupo madiwani wapya kama robo tatu hivyo hatufahamu miradi hiyo — mjadala utawezekanaje?” alisema Chanila.
Katika kikao hicho pia, Constantine Sima alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza baada ya kupata kura zote 26 (100%), huku Anita Rwezaura akichaguliwa kuwa Naibu Meya kwa kura hizo hizo.
Akijibu hoja za madiwani, Mstahiki Meya Sima alisema halmashauri itaandaa kikao maalumu cha semina elekezi kwa madiwani wote. Pia alibainisha kuwa zoezi la kuunda kamati za kudumu linaendelea ili kuhakikisha kila diwani anashiriki ipasavyo katika kusimamia shughuli za kimaendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, amewataka madiwani kusaidia kusimamia kwa uadilifu miradi ya maendeleo kwa kuwa wananchi wamewaamini na kuwachagua kwa matarajio ya kuona mabadiliko chanya.
Amesema ni muhimu kwa madiwani kufahamu fursa na changamoto zilizopo katika maeneo yao ili washiriki kikamilifu katika kusukuma mbele juhudi za maendeleo.
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, John Nzilanyingi, alishukuru kwa ushindi alioupata na kuipongeza halmashauri kwa kuwa na madiwani wengi vijana wasomi, akisema hatua hiyo italeta hamasa mpya katika kukuza uchumi wa jiji.
Aidha, aliwataka madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wa Jiji ili kutimiza matarajio ya wananchi wa Mwanza na Taifa kwa ujumla.


