Na Suleiman Shagata – Mwanza
Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali za mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, na kuachana na kilimo kisicholeta tija.
Wito huo umetolewa leo jijini Mwanza na watumishi wa TADB wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma na fursa zinazotolewa na benki hiyo kwa jamii, zikiwa na lengo la kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi kwenye kilimo cha kisasa na cha kibiashara.
TADB Yazidi Kusogeza Huduma Kwa Wakulima wa Kanda ya Ziwa
Meneja wa TADB Kanda ya Ziwa, Alphonce Mokoki, alisema Kanda ya Ziwa ni kitovu kikubwa cha uzalishaji nchini, ambapo huzalishwa mazao ya kimkakati kama pamba, kahawa, mpunga, mahindi, mbaazi na maharage.
Aidha, eneo hilo ni maarufu kwa ufugaji wa samaki, ng’ombe na kuku, hali inayoifanya kuwa sehemu muhimu kwa uwekezaji wa kifedha kupitia mikopo ya TADB.
Mokoki alibainisha kuwa benki hiyo imejipanga kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wakulima kwa wakati, huku akiwasisitiza waandishi wa habari kuendelea kuibua fursa na kuhamasisha matumizi ya huduma hizo ili kubadilisha mfumo wa kilimo nchini.
TADB Yatoa Zaidi ya Bilioni 631 kwa Miradi ya Kilimo
Afisa Masoko wa TADB, Richard Sempindu, alisema tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2015, tayari imeshatoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 631 kwa miradi 151 nchini.
Kwa upande wa Mkoa wa Mwanza pekee, zaidi ya bilioni 79 zimetolewa kwa miradi 61, huku lengo likiwa ni kuwawezesha wakulima, wavuvi na wafugaji kuhamia kwenye kilimo cha kibiashara na kuongeza usalama wa chakula nchini.
Sempindu aliongeza kuwa kupitia mpango wa kuhamasisha vijana na wanawake, TADB imetoa mikopo yenye thamani ya bilioni 12.4 kwa vikundi 120 katika Kanda ya Ziwa ikiwa na wanufaika 1,904 waliowezeshwa kuanzisha ufugaji wa samaki kwa mfumo wa vizimba.
RC Mtanda: “Mimi ni Miongoni mwa Walionufaika”
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliipongeza TADB kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wanahabari, akisema yatasaidia kuwafikia watanzania wengi kupitia vyombo vya habari.
Mtanda alifichua kuwa yeye mwenyewe ni miongoni mwa walionufaika na huduma za TADB, na kuwataka wakulima kutumia fursa hiyo kubadilisha kilimo chao kuwa na tija zaidi.
Aidha, aliwataka waandishi wa habari kutumia fursa zinazotolewa na TADB kuanzisha miradi yao, ikiwemo ufugaji wa samaki wa vizimba, ili kujiongezea kipato kupitia kilimo na ufugaji.
Bilioni 7.5 Zawanufaisha Vijana na Wanawake Mwanza
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, TADB imetoa zaidi ya bilioni 7.5 kwa vikundi mbalimbali mkoani Mwanza. Walionufaika ni pamoja na:
Vyama 14
Vikundi binafsi 12
Kampuni 4
Vijana 350, wakiwemo wanawake 227, kupiti
a Mradi wa Kuongeza Ajira kwa Vijana (BBT)


