Jeshi la Polisi Tanga Lajipanga Kuimarisha Usalama Kuelekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya

Xmation Media
By -
0

 


Jeshi la Polisi Tanga Lajipanga Kuimarisha Usalama Kuelekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya

Na Agnes Mambo, Tanga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limejipanga kikamilifu kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia pamoja na mali zao unaimarika katika kipindi hiki cha kuelekea kilele cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema jeshi hilo limeimarisha doria za miguu na magari katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu ili kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Doria Zaimarishwa Maeneo Muhimu

Kamanda Mchunguzi amesema doria zitafanyika kwa nguvu zaidi katika:

  • Nyumba za ibada

  • Vituo vya mabasi

  • Masoko

  • Fukwe za bahari

  • Kumbi za starehe

  • Maeneo ya makazi ya wananchi

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu kwa amani na usalama bila hofu ya vitendo vya kihalifu.

Wito kwa Wananchi Kuzingatia Tahadhari za Usalama

Jeshi la Polisi limewakumbusha wananchi kuzingatia kanuni ya msingi ya kiusalama inayosema “usalama unaanza na mtu mwenyewe.” Kamanda Mchunguzi amesisitiza wananchi kuhakikisha hawayaachi makazi yao bila uangalizi, hususan kipindi hiki cha sikukuu.

Mafanikio Kupambana na Ukatili Dhidi ya Watoto

Kuelekea msimu huu wa sikukuu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kushughulikia matukio makubwa ya ukatili dhidi ya watoto.

Kamanda Mchunguzi amesema kuwa mnamo tarehe 08 Oktoba, 2025, katika kijiji cha Kiloza, wilayani Korogwe, mtoto mmoja mwenye umri wa miaka mitatu (3) alijeruhiwa vibaya baada ya kukatwa mguu wa kulia kwa kitu chenye makali.

Uchunguzi ulibaini kuwa mtuhumiwa Abraham Yonathani Shelutete alifanya kitendo hicho kutokana na wivu wa mapenzi. Baada ya ushahidi kuwasilishwa mahakamani, mtuhumiwa alipatikana na hatia mnamo 19 Novemba, 2025, na kuhukumiwa:

  • Kifungo cha miaka saba (07) gerezani

  • Kulipa fidia ya Tsh 100,000/= kwa mhanga

Mtuhumiwa Mwingine Afikishwa Mahakamani

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga mnamo 24 Disemba, 2025 limemfikisha mahakamani mtuhumiwa Isaka Clement Ngulizi, mkazi wa Welei, kwa kosa la kumshambulia na kumkata vidole vitatu mwanafunzi wa darasa la nne mwenye umri wa miaka 11.

Tukio hilo lilitokea tarehe 02 Disemba, 2025, ambapo mtuhumiwa alidai kumkuta mtoto huyo akijaribu kuiba ndani ya nyumba yake.

Polisi Yatoa Onyo Kali kwa Wananchi

Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa wananchi kuwa kujichukulia sheria mkononi ni kosa la jinai, na hakuna sababu yoyote itakayokubalika kisheria kwa kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya mtu mwingine.

Wito kwa Wazazi, Watumiaji wa Barabara na Jamii kwa Ujumla

Kutokana na mazingira ya matukio hayo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa:

  • Wazazi na walezi kuongeza ulinzi na uangalizi kwa watoto wadogo

  • Kuepuka kuwaacha watoto kutembea peke yao bila uangalizi wa mtu mzima

  • Watumiaji wa barabara kuzingatia sheria, kuepuka ulevi na mwendo kasi

Doria Kali Maeneo ya Starehe na Barabara Kuu

Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa doria zitakuwa kali katika maeneo yote ya starehe na barabara kuu zinazoingia na kutoka Mkoa wa Tanga ili kuhakikisha amani na utulivu vinatawala wakati wa sikukuu.

Jeshi hilo linaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, na linawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za haraka kuhusu viashiria vya uvunjifu wa amani kupitia namba za dharura au kituo chochote cha polisi kilicho karibu.







Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default