Na Suleiman Shagata, Mwanza
Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko la Mchafukuoga, Kata ya Igogo, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, wameelezea malalamiko yao kuhusu hatua ya baadhi ya wenzao kurejea kufanya biashara katikati ya Jiji—eneo ambalo awali waliondolewa ili shughuli zifanyike katika masoko rasmi.
Katibu Msaidizi wa soko hilo, Peter Osuju, alisema uamuzi wa serikali kuwaondoa wafanyabiashara kwenye maeneo yasiyo rasmi na kuwapeleka kwenye masoko maalumu ulikuwa mzuri na uliisaidia Halmashauri ya Jiji kuwa na mpangilio bora wa maeneo ya biashara.
Hata hivyo, Osuju alionesha masikitiko yake juu ya hali ya sasa ambapo baadhi ya wafanyabiashara wamerudi katika maeneo yasiyo rasmi kama Makoroboi, Barabara ya Nyerere na Soko Kuu, jambo ambalo limepunguza idadi ya wanunuzi wanaofika Mchafukuoga.
“Dhamira ya maslahi ya kitaifa isiharibiwe na masuala ya kisiasa. Kwanini wengine waruhusiwe kurudi katikati ya Jiji, sehemu ileile tulikoondolewa?” alisema Osuju.
Amesema kuwa wanaiomba Halmashauri ya Jiji kuchukua hatua na kuhakikisha wafanyabiashara wote wanarudi kwenye masoko rasmi yaliyotengwa zaidi ya miaka minne iliyopita, kwani kwa sasa wanapata hasara kutokana na kukosa wateja.
Changamoto ya Mikopo ya Serikali
Osuju aliongeza kuwa licha ya kukamilisha taratibu zote za kupata mikopo ya serikali kupitia makundi ya kiuchumi, bado amekuwa akizungushwa na taasisi za kifedha bila kupata majibu ya uhakika.
Wito wa Ujenzi wa Soko la Kisasa
Mfanyabiashara mwingine, Elimokozi Matemba, alilaani kitendo cha baadhi ya wafanyabiashara kurudi kufanya biashara katikati ya Jiji badala ya kuendelea kutumia soko walilopewa.
Ameiomba serikali kutenga bajeti ya kujenga soko la kudumu na la kisasa katika eneo hilo ili kuwaondolea hofu na kuwapa uhakika wa kufanya shughuli zao bila kuhamishwa mara kwa mara.
Aidha, amesema utaratibu wa marejesho ya mikopo ya serikali uwe rafiki kwa wafanyabiashara wadogo kwani urejeshaji wa haraka unawafanya washindwe kukua na kupata faida.
Wafanyabiashara Wanataka Usimamizi Madhubuti
Mfanyabiashara mwingine, Judith Kaino, alieleza kuchanganyikiwa na hatua ya baadhi ya wafanyabiashara kurudi mjini, huku wao wakiachwa pembezoni bila wateja.
Amesema miaka minne imepita tangu waondolewe mjini, lakini hali ya kutorudi kwa wenzao kwenye soko rasmi inawafanya wapate hasara kubwa.
“Nataka serikali ituambie kama hapa ni eneo la kudumu ili niweze kutengeneza kibanda imara,” alisema.
Mwingine aliyeomba jina lake lihifadhiwe alidai kuwepo kwa upendeleo, kwani wanaorudi mjini wanachukua wateja wote, huku wao wa Mchafukuoga wakibaki bila mauzo ya kutosha.
.png)
.png)


.png)
.png)
