Na Suleiman Shagata, Mwanza
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Mwanza limewataka waumini na Watanzania kwa ujumla kuendeleza upendo na umoja uliodumu nchini kwa miaka mingi, na kutokubali kugawanywa kwa misingi ya dini.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Mwanza katika sherehe za Maulid zilizofanyika katika Msikiti wa Shamsiya, Kirumba, Manispaa ya Ilemela, ambapo mashehe na viongozi mbalimbali walipata fursa ya kuhimiza amani na mshikamano.
Tanzania Ina Historia ya Umoja – Sheikh Kabeke
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, alisema Tanzania imejengeka katika misingi ya umoja na mahusiano mazuri kwa muda mrefu, hivyo ni muhimu kuendelea kulinda misingi hiyo.
Aliwaonya wananchi kutokubali kupandikizwa propaganda zinazolenga kujenga chuki kwa misingi ya kidini, hasa kufuatia matukio ya machafuko yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali.
> “Nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda tume ya usuluhishi ili kuchunguza kiini cha machafuko na kutafuta suluhisho la kudumu,” alisema Sheikh Kabeke.
Vijana Waonywa Kutotumiwa Vibaya – DC Ilemela
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, aliwataka Waislamu kuishi kwa kufuata maadili ya dini yanayosisitiza upendo, amani na uvumilivu.
Alisema Watanzania wanategemeana, hivyo ukabila na misingi ya dini havipaswi kuwa chanzo cha mgawanyiko.
> “Baadhi ya watu wanawachochea vijana wakiwa nje ya nchi. Acheni kutumiwa kwa maslahi ya watu wachache,” alisema Mkalipa.
Heshima na Maadili Kwa Vijana – Sheikh Juma
Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Juma Abdul Walith Juma, aliwataka vijana kurejea kwenye maadili ya Kitanzania, ikiwemo heshima kwa wazazi na wakubwa.
Alisema kuzingatia maadili kutawasaidia kujiepusha na ushawishi mbaya na kuwa tayari kupokea hekima wanazoelekezwa.
Pia alisisitiza umuhimu wa kulinda amani ya taifa kwani ikipotea, jamii itaishi kwa hofu na kushindwa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za uzalishaji.
Amani na Mshikamano Ni Msingi – Mashehe Watoa Wito
Sheikh Sululu Salum wa Msikiti wa Shamsiya alisema Watanzania wote wanapaswa kupendana na kuondoa tofauti ili kujenga taifa linaloishi kwa umoja na imani moja bila hofu.
Naye Sheikh Abuu Jadawi, msemaji wa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alisoma maandiko ya Qur’an Tukufu na kuwataka waumini kuyafuata kwa kuwa ndiyo yanayoongeza hekima na maadili.
> “Maandiko ya Mtume ni neema kwa Waislamu, hasa katika kipindi hiki cha Maulid,” alisema Sheikh Jadawi.
Uzalendo na Amani Yaendelea Kusistizwa
Sheikh Issa Masanja, aliyemwakilisha Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, alihitimisha kwa kuwataka Watanzania kutunza amani, kupenda nchi yao, na kuwa na uzalendo
wa dhati ambao ni msingi wa maisha ya binadamu.







