WAZIRI MKUU MAJALIWA AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUKEMEA UVUNJIFU WA MAADILI NA KULIOMBEA TAIFA AMANI
Na Agnes Mambo, Xmation Media – Tanga
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, ametoa wito kwa viongozi wa dini kote nchini kuendelea kukemea vitendo vya uvunjifu wa maadili na kuliombea taifa amani, hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza katika Baraza la Maulid Kitaifa la kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), lililofanyika wilayani Korogwe mkoani Tanga, Waziri Mkuu amesema viongozi wa dini wana nafasi ya kipekee katika jamii na kauli zao zina nguvu kubwa ya kuhimiza maadili mema.
Aidha, Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini pamoja na viongozi wake kuanzia ngazi za msingi hadi taifa, ili kuhakikisha changamoto za kijamii zinajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi wa pamoja.
Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakary Zubeir, amewataka viongozi wa dini kusimamia amani katika maeneo yao, akibainisha kuwa jukumu hilo ni sehemu ya mafundisho ya dini na maelekezo ya Mtume Muhammad (S.A.W).
Amesisitiza pia umuhimu wa viongozi na waumini kutokufumbia macho viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani. Aidha, Mufti amewahimiza Waislamu na wananchi kwa ujumla kujitokeza kusikiliza sera za wagombea wa vyama mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ameishukuru Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kuchagua mkoa wa Tanga kuwa mwenyeji wa Baraza la Maulid Kitaifa. Amesema Tanga itaendelea kuwa mfano wa mshikamano, amani na utulivu kwa wananchi wake.





