DOYO Aahidi Kiwanda cha Kisasa cha Mkonge na Mikopo Bure kwa Wananchi
Na, Agnes Mambo – Xmation media Tanga
Akihutubia wakazi wa Korogwe, mkoani Tanga, Doyo alisema kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, atahakikisha zao la mkonge linakuwa kati ya mazao yanayoitangaza Tanzania kimataifa na kuongeza kipato cha wananchi.
“Haiwezekani tuendelee kuteseka wakati zao la mkonge lina uwezo wa kutuletea maendeleo sisi na vizazi vyetu. Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kulitumia ipasavyo. Tarehe 29 Oktoba nendeni mkachague NLD na kunipa ridhaa ya kuwa Rais ili nihakikishe mnajinasua na umasikini kupitia zao hili,” alisema Doyo.
Ameahidi kujenga kiwanda cha kisasa cha mkonge na kusambaza pembejeo za kilimo bure kwa wakulima wa wilaya hiyo ili kuongeza tija.
Mbali na kilimo, Doyo pia ameahidi kupiga marufuku taasisi zinazotoa mikopo yenye riba kubwa, akisema imekuwa mzigo kwa wananchi hususan wanawake. Badala yake, aliahidi mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri itatolewa bure bila marejesho.
> “Wananchi wamekuwa wakidhalilishwa na mikopo umiza. Nitakapochaguliwa kuwa Rais, nitafuta kabisa mikopo hiyo na kuimarisha mikopo ya Halmashauri ambayo itatolewa bure kwa wakina mama, vijana na walemavu,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa NLD, Ibrahimu Pogora, alisema ilani ya chama hicho inalenga kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa hali ya chini, akibainisha kuwa chama tawala kimeshindwa kutatua kero za msingi katika sekta za kilimo, afya, ardhi na elimu kwa kipindi cha miaka 64 ya uhuru.
> “Watanzania tusifanye kosa tena. Tumeamini kwa miaka mingi lakini bado hatujaona maendeleo ya kweli. Tarehe 29 Oktoba, tupeni nafasi NLD ili tuwaletee maendeleo ya kweli,” alisema Pogora.




