PROF. MSOFE AFURAHISHWA NA MBEGU ZA ASA ZINAZOVUMILIA UKAME NA MVUA NYINGI

Xmation Media
By -
0

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msofe, amefurahishwa na aina za mbegu zinazozalishwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), zikiwemo mbegu zenye uwezo wa kustahimili ukame na mvua nyingi, hatua inayoweza kuwasaidia wakulima kuendelea kuzalisha katika mazingira tofauti ya hali ya hewa, ikiwemo kipindi cha mvua za El Niño hivyo kuleta usalama wa chakula hapa nchini.


Profesa Msofe ameonesha kufurahishwa na taarifa hizo Oktoba 13, 2026, alipotembelea banda la ASA katika maadhimisho ya kitaifa kuelekea Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.

Akiwa katika banda hilo, amepata maelezo kuhusu mbegu ya mahindi aina ya T105, ambayo ina uwezo wa kutoa mavuno ya magunia 18 hadi 22, kulingana na ukubwa wa eneo na masharti ya uzalishaji, huku ikiwa na uwezo wa kustahimili ukame na mvua nyingi.


Akitoa maelezo kuhusu mbegu hiyo, Afisa Masoko wa ASA, Suzan Ludovick, amesema mbegu hizo zinauzwa katika maonesho ya wiki ya maadhisho ya siku ya  chakula ili kuongeza usalama wa chakula ikiwemo mbegu ya T105 ni mbegu ya uchavushaji huria inayoweza kutoa mahindi mawili kwa kila mmea, hivyo kuwapa wakulima fursa ya kuongeza uzalishaji wanapozingatia kanuni bora za kilimo.

Amesema uwezo wa mbegu hiyo kustahimili mazingira tofauti ya upatikanaji wa maji unaifanya kuwa miongoni mwa chaguo zinazoweza kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwemo vipindi vya ukame na mvua nyingi jambo ambalo litaongeza chakula kwenye familia.


Katika hatua nyingine, Profesa Msofe amepata maelezo kuhusu mbegu ya mpunga aina ya SARO 5, ambayo huzalisha magunia 30 hadi 40 kwa ekari, kulingana na mazingira na usimamizi wa shamba.



Suzan amesema SARO 5 inafaa kwa kilimo cha mpunga katika maeneo ya mabondeni na inakubalika katika soko la mchele kutokana na harufu yake nzuri, sifa inayoweza kuongeza mvuto wa zao hilo kwa walaji.


Amesema matumizi ya mbegu bora zinazofaa katika mazingira ya wakulima, yakichanganywa na kuzingatia kanuni bora za kilimo, ni muhimu katika kuongeza tija, kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuboresha kipato cha wakulima.


Juhudi hizo zinatarajiwa kuendelea kuchochea matumizi ya mbegu bora, kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa chakula nchini.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default