Na Agnes Mambo, Mkinga
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, anayeshughulikia Uenezi, Mafunzo na Itikadi, Ndugu Kenan Kihongosi, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa nyumba za watumishi wa chama ambapo kila Wilaya imepangiwa kujenga nyumba nne, na kufanya jumla ya nyumba 36 zinazotarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kichama ya siku mbili Mkoani Tanga, Kihongosi alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Ndugu Rajab Abdul Rahman Abdallah, kwa juhudi zake katika kuhakikisha watumishi wa chama wanapata makazi bora na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Kihongosi alisema ujenzi wa nyumba hizo ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya kazi na ustawi wa watumishi wa chama katika ngazi za Wilaya.
Akiwa Wilayani Mkinga, Kihongosi pia alisisitiza umuhimu wa wananchi na wanachama kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano, akieleza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa.
Aidha, alizungumzia maendeleo ya miundombinu ya maji katika Mkoa wa Tanga, akisema kuwa yameendelea kuimarika kutokana na uwekezaji na fedha zinazotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kihongosi aliwataka wananchi wa Mkinga kuendelea kushirikiana na kukiamini Chama Cha Mapinduzi katika shughuli za maendeleo, huku akieleza kuwa CCM kinaendelea kuwa chama chenye nguvu katika Mkoa wa Tanga.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Rajab Abdul Rahman Abdallah, ametajwa kuchangia kiasi cha Shilingi bilioni 1 katika ujenzi wa nyumba za watumishi wa chama.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, tathmini ya gharama za ujenzi wa nyumba hizo inakadiriwa kufikia takribani Shilingi bilioni 2.5 hadi kukamilika kwake.
Ziara hiyo ya Kihongosi Mkoani Tanga ni sehemu ya shughuli za kichama zinazolenga kufuatilia utekelezaji wa miradi na kuimarisha shughuli za chama katika ngazi mbalimbali.




