Na Ashton Balaigwa, MOROGORO
Mradi wa kuongeza uwezo wa kusimamia Sera za Uchumi Jumuishi (IGE), unaofanya kazi katika nchi tano za Bara la Afrika, umesaidia Tanzania kuchochea ukuaji wa uchumi, uandaaji wa ajira, pamoja na ulinzi na urejeshaji wa mazingira na maliasili.
Mradi wa IGE, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), unafanya kazi katika nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Ethiopia, na umesaidia kukuza uchumi katika nchi hizo kwa kutatua changamoto mbalimbali.
Msimamizi Mkuu wa Mradi huo kwa upande wa Tanzania, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Aloyce Hepelwa, amesema mradi huo umesaidia kukuza uchumi baada ya kushirikisha viongozi wa Serikali na watafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam bila kuharibu mazingira.
"Mradi huu umekuja kuondoa vikwazo kati ya watafiti na watunga sera. Sisi tunafanya tafiti kwa sasa na watumishi wa Serikali kuchambua vitu vilivyopo Serikalini ambavyo vinaleta shida katika kukuza uchumi, kusudi kwa pamoja turekebishe tukiwa pamoja nao, na tumefanikiwa katika kukuza uchumi," alisema Hepelwa.
Amesema mradi huo ulianza kwa kuchambua vitu vilivyopo Serikalini vinavyoleta shida katika kukuza uchumi na kuvirekebisha ili kuleta mabadiliko, maendeleo na uchumi endelevu.
Ameongeza kuwa mradi huo, unaotekelezwa kupitia Shule Kuu ya Uchumi ya Chuo Kikuu hicho, unatumia rasilimali ikiwemo maji, misitu, madini na kilimo ili kuleta ukuaji wa uchumi.
Dk Hepelwa amesema awali waliona hakuna maana ya watafiti kukaa peke yao na kufanya utafiti bila kushirikiana na watunga sera waliopo Serikalini, hivyo mradi huo ukaja kuondoa tatizo hilo kwa kuwakutanisha wanataaluma na watunga sera ili kuleta maendeleo endelevu bila kuathiri mazingira.
Naye Mtafiti Mwandamizi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini, Mhandisi Dk Befrina Igulu, alisema wamekuwa wakishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye masuala ya tafiti ambazo wanazitumia katika kutekeleza programu zao za mazingira na usimamizi wa rasilimali za mazingira.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira, Wizara ya Kilimo, Dk Rose Mbezi, amesema umuhimu wa kilimo Barani Afrika hauwezi kupuuzwa licha ya kuwepo athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema licha ya athari hizo kuleta changamoto, kwa sasa zinatoa fursa mpya hasa kwa sekta ya kilimo ambayo ndiyo nguzo kuu ya uchumi wa nchi nyingi za Afrika, kwa kuwa inakadiriwa asilimia 70 ya Waafrika hutegemea kilimo kwa maisha yao.
Mwisho
Maelezo Picha: Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kusimamia Sera za Uchumi Jumuishi (IGE), kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Aloyce Hepelwa, akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro kuhusu mradi huo. Picha na Ashton Balaigwa, Morogoro.
