Na Agnes Mambo, Horohoro – Tanga
Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Mpakani cha Horohoro–Lungalunga kimeendelea kuandika historia mpya baada ya kurekodi ongezeko kubwa la biashara na makusanyo ya mapato, hali inayoonyesha kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya.
Akitoa taarifa ya utendaji wa kituo hicho mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bi. Annet Semwamba, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Horohoro (OSBP), Shadrack Mbonea Kavuta alisema thamani ya bidhaa zinazoingia kupitia kituo hicho imeongezeka kutoka shilingi bilioni 306.4 mwaka wa fedha 2022/23 hadi kufikia shilingi bilioni 548.8 mwaka wa fedha 2024/25.
Aidha, alisema katika mwaka wa fedha 2025/26, thamani ya bidhaa zilizoingia kupitia kituo hicho tayari imefikia shilingi bilioni 489.5, jambo linaloendelea kuashiria ukuaji wa biashara ya mipakani kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wa bidhaa zinazotoka nchini, Kavuta alisema thamani yake imeongezeka kutoka shilingi bilioni 134.7 mwaka 2022/23 hadi kufikia shilingi bilioni 175.9 mwaka 2025/26.
Alieleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano mzuri kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), ambao umeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kurahisisha biashara ya mipakani.
Hata hivyo, alisema kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa umeme wa uhakika pamoja na vifaa vya kuzimia moto. Aliiomba Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana na wadau kuhakikisha miundombinu hiyo inaboreshwa ili kuongeza usalama na ufanisi wa huduma.
Kavuta alibainisha kuwa Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Horohoro kinajumuisha taasisi 19 za Serikali zinazotoa huduma chini ya uratibu wa TRA, zikiwemo Idara ya Uhamiaji, TMDA, TAWA, Polisi, JWTZ, Zimamoto, TASAC, TFS, Tume ya Madini, GCLA pamoja na taasisi nyingine muhimu.
Alisema majukumu makuu ya kituo hicho ni pamoja na kukusanya mapato ya Serikali, kurahisisha biashara ya mipakani, kudhibiti magendo, kulinda jamii dhidi ya bidhaa hatarishi, kutekeleza mikataba ya kimataifa ya biashara na kuhifadhi takwimu za biashara.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bi. Annet Semwamba, alisema ameridhishwa na mafanikio yaliyopatikana katika Kituo cha Horohoro, hususan ongezeko la biashara na bidhaa zinazopita kupitia mpaka huo.
Aliwapongeza watumishi wa kituo hicho kwa kazi nzuri wanayoifanya na kusisitiza kuwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutatua changamoto zilizopo ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha biashara na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama.
Kwa kasi hii ya ukuaji wa biashara, Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Horohoro kinaendelea kuwa moja ya lango muhimu la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, kikichochea maendeleo ya uchumi na ushirikiano wa kikanda.