Morogoro
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Maswi, ametembelea Makazi ya Wazee Fungafunga yaliyopo mkoani Morogoro kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zinazotekelezwa na wazee wanaoishi katika makazi hayo.
Katika ziara hiyo, Maswi alipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali inayowawezesha wazee kujishughulisha na shughuli za kiuchumi, ikiwemo ufugaji wa kuku, kilimo cha mbogamboga na utengenezaji wa mikeka kwa njia ya ufumaji. Shughuli hizo zimeendelea kuwapatia wazee kipato, kuchangia ustawi wa uchumi wao pamoja na kuwasaidia kufanya mazoezi ya viungo kupitia kazi wanazozifanya kila siku.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Maswi alieleza kuridhishwa na namna makazi hayo yanavyowahamasisha wazee kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali ambazo zinaongeza tija na kuboresha maisha yao.
Aidha, amewapongeza watumishi wa Makazi ya Wazee Fungafunga kwa kujituma katika kuwalea, kuwahudumia na kuhakikisha wazee wanaishi katika mazingira salama na yenye heshima, huku wakiendelea kushiriki katika shughuli zinazowajengea afya na kujitegemea.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum za kufuatilia utekelezaji wa huduma za ustawi wa jamii na kuhakikisha makundi maalum yanapata huduma bora pamoja na fursa za kushiriki katika shughuli za maendeleo.