Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba ya Dhahabu) yameendelea kuvutia mamia ya wananchi wanaofika kujifunza na kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma na binafsi.
Leo, Julai 1, 2026, Banda la Wizara ya Nishati lilianza siku kwa kumpokea mgeni wake wa kwanza, Bi. Ester Mashaka Msengi, mkazi wa Kibaha Mjini, mkoani Pwani.
Katika ziara yake, Bi. Ester alipata elimu kuhusu Nishati Safi ya Kupikia kutoka kwa Mtaalam wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Bi. Amina Almasi, chini ya uangalizi wa Mhandisi wa Nishati, Zahoro Rashid.
Baada ya mafunzo hayo, Bi. Ester alieleza kuridhishwa na elimu aliyopata, akibainisha kuwa maarifa hayo yatamsaidia kuelewa kwa kina manufaa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta ya nishati.
Wizara ya Nishati inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake lililopo karibu na jengo la TANESCO, katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam, ili kujifunza kuhusu huduma, miradi na fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta ya nishati.
Tembelea Banda la Wizara ya Nishati leo na ujionee teknolojia, huduma na suluhisho mbalimbali vinavyoendelea kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini.
#SabasabayaDhahabu2026 #WizarayaNishati #Day4