Wakulima 6,000 Morogoro na Iringa Waongeza Uzalishaji Kupitia Mbinu za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
Wakulima zaidi ya 6,000 wa mazao ya mpunga, alizeti, miwa, soya na kokoa kutoka mikoa ya Morogoro na Iringa wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mazao yao baada ya kupata mafunzo ya mbinu bora za kilimo zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mradi wa SUSTAIN PRO, unaolenga kuendeleza mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula nchini Tanzania na Msumbiji, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Serikali ya Norway.
Kwa mujibu wa Afisa Programu wa IUCN, Samuel Kajiba, asilimia 83 ya wakulima waliopatiwa mafunzo walitumia maarifa hayo kwa vitendo na kufanikiwa kuongeza tija mashambani.
Katika zao la mpunga, wakulima wa Malinyi, Mlimba na Ifakara wameongeza uzalishaji kutoka wastani wa gunia 5 hadi gunia 15 kwa ekari. Kwa upande wa miwa wilayani Kilosa, uzalishaji umeongezeka kutoka tani 47 hadi tani 50 kwa hekta.
Mazao ya alizeti na soya katika wilaya za Kilolo na Iringa yameonyesha mafanikio makubwa zaidi baada ya mavuno kuongezeka kutoka kilo 300–400 hadi kufikia kilo 800 kwa ekari.
Mafunzo yaliyotolewa yalihusisha matumizi ya mbegu bora, kilimo shadidi, umwagiliaji, matumizi sahihi ya pembejeo, mbolea za asili, mzunguko wa mazao pamoja na kilimo mseto kinachochanganya mazao na miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.
Akizungumza katika mdahalo uliowakutanisha wakulima na wadau wa kilimo, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano wa COPRA, Theresia Christian, alisema mamlaka hiyo inaendelea kusimamia uzalishaji endelevu wa mazao pamoja na kusaidia upatikanaji wa masoko kupitia mifumo ya kidijitali na kilimo cha mkataba.
Aidha, alisema serikali itaendelea kutoa ruzuku za pembejeo na mbegu bora, hasa za alizeti, ili kuongeza uzalishaji na kusaidia Tanzania kufikia lengo la kujitosheleza kwa mafuta ya kula.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mpunga Wilaya ya Malinyi, Erkus Ngapulila, alisema matumizi ya teknolojia ya kitalu mkeka yamewawezesha kuongeza mavuno kutoka gunia 26 hadi gunia 42 kwa ekari moja.
Mafanikio haya yanaonyesha namna mafunzo sahihi, teknolojia za kisasa za kilimo na ushirikiano wa wadau mbalimbali vinavyoweza kuongeza uzalishaji wa mazao huku vikisaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.