TRA Yatimiza Miaka 30: Makusanyo Yaongezeka Kutoka Bilioni 531 hadi Trilioni 32
Na Agnes Mambo | Xmation Media Tanga
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, ikijivunia mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Makusanyo yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 531 mwaka wa fedha 1996/1997 hadi kufikia Shilingi trilioni 32 katika mwaka wa fedha 2025/2026, na kuvuka malengo yaliyowekwa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo mkoani Tanga, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema Serikali imefanikiwa kudhibiti uingizaji wa bidhaa za magendo kupitia bandari bubu kutokana na kuimarishwa kwa doria, utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara na ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya ulinzi na usalama, TRA pamoja na wadau wa biashara.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, CPA Castro John, amesema ongezeko hilo kubwa la mapato limetokana na matumizi ya teknolojia, maboresho ya mifumo ya ukusanyaji kodi, kuongezeka kwa elimu kwa walipa kodi na ushirikiano mzuri kati ya TRA na wafanyabiashara.
Amesema TRA itaendelea kuwekeza katika teknolojia, kupanua wigo wa walipa kodi na kuboresha huduma kwa wananchi ili kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania.