SEMINA YAFICHUA UKATILI WA KIJINSIA UNAOWAKABILI WAFANYAKAZI WA NYUMBANI TANZANIA

Xmation Media
By -
0
Wafanyakazi wa nyumbani nchini Tanzania wameendelea kuibua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika mazingira yao ya kazi, huku ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono vikitajwa kuwa miongoni mwa matatizo makubwa yanayohatarisha usalama, utu na afya zao ya kimwili pamoja na kisaikolojia.

Hali hiyo imebainishwa wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa nyumbani kuhusu haki zao za msingi, iliyoandaliwa chini ya mradi wa Chama cha Wafanyakazi (CWM) Jimboni Morogoro unaolenga kuwapatia wafanyakazi wa nyumbani mafunzo ya kuongeza ujuzi na kuwajengea uwezo wa kutambua na kudai haki zao kazini.

Washiriki wa semina hiyo walieleza kuwa licha ya mchango mkubwa wanaoutoa katika familia wanazozihudumia, wengi wao bado wanakumbana na mazingira magumu ya kazi, ikiwemo mishahara midogo, kazi nyingi zisizoendana na makubaliano ya awali, pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyofanywa na baadhi ya waajiri au wanafamilia wa waajiri wao.

Miongoni mwa washiriki hao ni Veronica Jonas, ambaye amekuwa akifanya kazi za nyumbani tangu mwaka 2020 akiwa mkoani Kigoma. Veronica alisema kuwa kazi za nyumbani zimemwezesha kujipatia kipato na kukidhi mahitaji yake muhimu ya maisha, lakini pia amekutana na changamoto nyingi zilizomfanya kutambua umuhimu wa kujua haki zake kama mfanyakazi.
Alisimulia kuwa wakati mmoja alikumbana na hali ya kutakiwa kimapenzi na baba mwenye nyumba aliyokuwa akimfanyia kazi. Kutokana na hofu ya usalama wake na kutaka kuepuka migogoro ndani ya familia hiyo, aliamua kuacha kazi na kuondoka bila kuchukua hatua yoyote ya kisheria.

Kwa mujibu wa Veronica, wakati huo hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu haki zake wala sheria zinazowalinda wafanyakazi wa nyumbani dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

“Nilichofanya ni kuondoka tu ili kujinusuru. Sikuwa najua kwamba kuna sheria zinazoweza kunilinda na kunisaidia kupata haki yangu. Kupitia mafunzo haya nimeelewa kuwa wafanyakazi wa nyumbani tuna haki sawa na wafanyakazi wengine na tunaweza kudai haki hizo kupitia sheria zilizopo,” alisema Veronica.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa waajiri kupewa elimu kuhusu haki za wafanyakazi wa nyumbani ili kuondoa mtazamo wa kuwaona kama watu wanaohitaji mshahara pekee bila kujali utu na heshima zao.

“Ningependa waajiri watambue kuwa nasi ni binadamu wenye haki na heshima. Kama wao wanavyopambana kupata mazingira bora ya kazi, mishahara mizuri na kupinga unyanyasaji katika maeneo yao ya kazi, nasi pia tunahitaji kuthaminiwa na kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili,” aliongeza.

Kwa upande wake, Witnes Joseph alisema alianza kufanya kazi za nyumbani mwaka 2020 baada ya wazazi wake kutengana na familia yao kubaki chini ya malezi ya bibi yake. Kutokana na hali ngumu ya maisha, alilazimika kuingia kwenye ajira za nyumbani ili kupata kipato cha kumsaidia mdogo wake kuendelea na masomo.

Witnes alisema licha ya yeye kushindwa kuendelea na elimu zaidi ya darasa la saba kutokana na ukosefu wa msaada, amejitolea kuhakikisha mdogo wake anapata fursa ya kutimiza ndoto zake za elimu. Kwa sasa mdogo wake anasoma kidato cha tatu, huku yeye akiendelea kufanya kazi kwa bidii ili kugharamia mahitaji yake.

Mbali na kumsaidia mdogo wake, Witnes pia amekuwa msaada kwa ndugu wengine wa familia, wakiwemo wanafunzi wa elimu ya juu wanaomtegemea wanapopata changamoto za kifedha.

Hata hivyo, safari yake ya kazi za nyumbani haikukosa vikwazo. Alieleza kuwa aliwahi kukumbana na unyanyasaji wa kingono kutoka kwa watoto wa mwajiri wake, hali iliyomlazimu kuacha kazi na kuhamia mkoani Morogoro kutafuta mazingira salama zaidi ya kuishi na kufanya kazi.

Kwa sasa, amesema anaishi kwa amani katika familia inayomheshimu na kuthamini mchango wake, huku akitarajia kujiendeleza zaidi kupitia mafunzo ya ufundi yanayotolewa kwa ushirikiano kati ya CWM na Chuo cha VETA Mikumi.

Washiriki wa semina hiyo wameeleza matumaini makubwa kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kutambua haki zao, kupambana na vitendo vya unyanyasaji na kujenga mustakabali bora wa maisha yao.

Wameitaka serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa wafanyakazi wa nyumbani, kuongeza elimu kwa waajiri na kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezwa kikamilifu ili kulinda kundi hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likifanya kazi muhimu kwa jamii lakini mara nyingi likikosa sauti ya kutetea haki zake.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default