Na Agnes Mambo,MUHEZA.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ameunda kamati maalumu ya kuchunguza mazingira yaliyozunguka utekelezaji wa amri ya mahakama uliohusisha uvunjaji wa nyumba za wananchi katika Kijiji cha Msakangoto, Kata ya Kigombe, Wilaya ya Muheza.
Akizungumza na waandishi wa habari, Balozi Batilda amesema Serikali ya Mkoa inahitaji kupata ufafanuzi wa kina kuhusu mchakato mzima wa kuwaondoa wananchi hao, hususan baada ya kubainika kuwa shughuli hiyo ilifanyika Mei 22, 2026 bila ushirikishwaji wa Jeshi la Polisi pamoja na viongozi wa Mkoa na Wilaya.
Amesema kamati hiyo itachunguza sababu za kutoshirikishwa kwa mamlaka husika wakati wa utekelezaji wa amri hiyo, pamoja na kubaini maandalizi yaliyofanyika kuhakikisha wananchi walioondolewa wanapata makazi mbadala na huduma muhimu za kijamii.
Balozi Batilda ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa ilifanya mazungumzo na wamiliki wa shamba la mkonge kuhusu utaratibu wa kuwaondoa wananchi hao kwa kuzingatia utu, ubinadamu na maslahi ya wananchi. Hata hivyo, utekelezaji uliofanyika bila taarifa kwa viongozi wa Serikali umeibua maswali mengi yanayohitaji majibu.
Aidha, amesema kamati hiyo itatathmini ubora wa eneo la ekari 37 lililotengwa kwa ajili ya makazi mapya ya wananchi hao pamoja na athari zinazoweza kujitokeza kwa familia zilizoishi eneo hilo kwa muda mrefu, ikiwemo watoto wanaopata huduma za elimu katika shule zilizopo jirani na makazi yao ya sasa.
“Hatupingi amri ya mahakama, lakini tunataka kujua utaratibu uliotumika, maandalizi yaliyofanyika na namna wananchi hawa watakavyoendelea na maisha yao katika maeneo mapya,” amesema Mhe. Burian.
Mkuu huyo wa Mkoa pia ametoa onyo kwa mtu au taasisi yoyote itakayotekeleza shughuli kama hizo bila kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka husika, akisisitiza kuwa ushirikishwaji ni muhimu katika kulinda amani, usalama na maslahi ya wananchi.
Kamati hiyo imepewa siku tano kuanzia Juni 1 hadi Juni 5, 2026 kukamilisha uchunguzi wake na kuwasilisha taarifa kwa Serikali ya Mkoa kwa hatua zaidi.
Wakati huo huo, Serikali ya Mkoa wa Tanga imeendelea kuchukua hatua za dharura kwa kuwapatia wananchi walioathirika maturubai kwa ajili ya kujikinga dhidi ya mvua wakati suluhisho la kudumu likiendelea kutafutwa.
.png)


