RC TANGA AHAMASISHA MICHANGO KUKAMILISHA UJENZI WA KITUO CHA MOYO KCMC

Xmation Media
By -
0


Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amewataka wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kuendelea kuchangia ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Tiba ya Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya KCMC ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.



Balozi Batilda alitoa wito huo wakati akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya mradi huo iliyofanyika tarehe 30 Mei 2026 na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi pamoja na wageni waalikwa mbalimbali.


Alisema kituo hicho kitakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kwenda nje ya nchi kwa matibabu.



Kwa mujibu wa Dkt. Burian, mradi huo una gharama ya takribani shilingi bilioni 50, ambapo bilioni 25 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo na bilioni 25 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na teknolojia za kisasa. 


Alibainisha kuwa hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 22 zimepatikana kupitia michango ya wadau mbalimbali huku kiasi cha takribani shilingi bilioni 3 kikihitajika kukamilisha sehemu ya ujenzi.


“Uwekezaji katika sekta ya afya ni uwekezaji katika maisha ya wananchi na maendeleo ya taifa. Kituo hiki kitakapokamilika kitasaidia kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania, wakiwemo watoto wenye changamoto za moyo tangu kuzaliwa,” alisema Dkt. Burian.


Aidha, aliwashukuru wadau wote waliojitokeza kuchangia mradi huo na kueleza imani yake kuwa ushirikiano uliopo utawezesha kukamilika kwa kituo hicho muhimu kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Prof. Gileard Masenga, alisema ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo na mishipa ya damu limeongeza mahitaji ya huduma za kibingwa za moyo nchini.


Alisema kwa miaka mingi wagonjwa wengi walilazimika kusafiri umbali mrefu au kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu ya moyo kwa gharama kubwa, hali iliyokuwa ikiathiri familia nyingi na uchumi wa taifa.


Prof. Masenga alieleza kuwa Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya KCMC itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 114 kwa wakati mmoja na itatoa huduma za kisasa ikiwemo uchunguzi wa kina, matibabu ya magonjwa ya moyo, upasuaji wa moyo, huduma za wagonjwa mahututi pamoja na ufuatiliaji wa muda mrefu kwa wagonjwa.


Alisema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia kuleta huduma za moyo karibu zaidi na wananchi wa Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine ya nchi huku kikipunguza utegemezi wa matibabu nje ya Tanzania.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default