WADAU WATAKA AMCOS KUSIMAMIA MAENDELEO YA USHIRIKA KWA JUHUDI KUBWA

Xmation Media
By -
0


NA SULEIMAN SHAGATA

MWANZA - Wadau wa maendeleo ya ushirika wamevitaka vyama vya msingi vya wakulima na Masoko (AMCOS) na vile vya ushirika kusimamia maendeleo yao kwa juhudi kubwa ili ziweze kuwaletea wananchi hali nzuri ya kiuchumi kwa haraka.

Hayo yamebainishwa jana Jijini Mwanza na wadau hao walipokuwa kwenye Mkutano Mkuu wa 34 wa Chama Kikuu Cha Ushirika Nyanza (1984) ambapo walisema maendeleo ya ushirika yanapashwa kuanzia kwenye ngazi za AMCOS.

Mrajis Asisitiza Ufuataji wa Kanuni

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Mwanza, Hilda Boniphace aliyemwakilisha Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Benson Ndiege, alisema ushirika kuweza kujiendesha kwa faida kunaleta tija kwa ukuaji wa sekta ya pamba hapa nchini.

Aliitaka Chama Cha Ushirika Nyanza (NCU 1984) Mkoani Mwanza kufanya jitihada za kuhakikisha kuwa wanafufua kiwanda cha kuchambua pamba kilichopo Wilayani Magu ili kianze kazi zake kwa sasa.

"Nimetumwa na Mrajis kuvitaka vyama vyote kufanya kazi zao kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu, kwa weledi mkubwa na kutatua baadhi ya changamoto zinazojitokeza ili kila bodi inayomaliza muda wake kuacha alama ya kukumbukwa," alisema Boniphace.

Mwelekeo wa Kidijitali katika Ushirika

Boniphace aliongeza kusema kuwa vilevile Mrajis wa Vyama vya Ushirika anavitaka vyama vya ushirika kujiendesha kwa kutumia mifumo ya kidijitali jumuishi katika kazi zao za kila siku ili ziweze kuwa na ufanisi.

Hatua hii inakuja wakati serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa teknolojia katika kuongeza tija na uwazi katika sekta ya ushirika nchini.

Mkuu wa Mkoa Apongeza Juhudi za NCU

Naye Katibu Tawala Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza, Maria Msengi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliipongeza NCU kwa kuendelea kusimamia malengo ya kuasisiwa kwa ushirika hapa nchini.

Alisema viongozi wa vyama vya ushirika wanapaswa kulinda kwa uaminifu na uadilifu mkubwa mali za ushirika ili ziweze kuendelea kuhudumia wanachama wake wanaoendelea kujiunga kila mara kwenye maeneo mbalimbali.

"Ili muweze kupiga hatua, Tume ya Maendeleo ya Ushirika iendelee kufanya ukaguzi mara kwa mara kwenye vyama vya ushirika," alisema Mtanda.

Elimu kwa Wakulima Muhimu

Aidha, Mtanda aliongeza kusema kuwa vyama vya ushirika vinapashwa kuendelea kutoa elimu kwenye jamii ya wakulima ili waweze kuleta mapinduzi makubwa kwenye kilimo chao katika maeneo yao.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya ushirika kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, na ulilenga kuboresha ufanisi wa huduma za ushirika kwa wakulima na jamii kwa ujumla.

Mkutano Mkuu wa 34 wa NCU uliandaliwa kwa lengo la kutathmini mafanikio ya mwaka uliopita na kuweka mkakati wa maendeleo ya vyama vya ushirika katika mwaka ujao.


Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default