Taa za Barabarani Zinawezesha Biashara za Usiku Katika Mwaka Mpya

Xmation Media
By -
0

 


Na Suleiman Shagata 

Mwanza - Wakaazi wa Mabatini Jijini Mwanza wameanza mwaka mpya kwa furaha baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja na barabara ya njia nne, huku wafanyabiashara wadogo wakichukua fursa ya taa za barabarani zilizofungwa kufanya biashara zao wakati wa usiku.

Wakaazi Wapumzika Baada ya Miaka ya Matatizo

Wakaazi wa eneo hilo wamesema kuwa awali walipata changamoto kubwa za mafuriko ya maji kwenye daraja ambayo yalisambaa hadi kwenye makazi yao na kusababisha vifo.



Easter Marco, muuzaji wa bidhaa mbalimbali katika mtaa wa Mabatini, ameshukuru serikali kwa kukamilisha mradi huo. "Tunamshukuru serikali yetu kwa kutufungia taa za barabarani hivyo kutuwezesha tufanya shughuli zetu hata usiku," alisema Marco.

Ufumbuzi wa Muda Mrefu kwa Tatizo la Mafuriko

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabatini Kaskazini, Hamis Nassoro, ameeleza kuwa mradi huu unaleta ufumbuzi wa muda mrefu kwa changamoto ya magari yanayoingia na kutoka Jijini Mwanza wakati wa mvua.

"Mafuriko yaliyokuwa yakitokea kwenye mto Milongo yalisababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Umahuri wa mkandarasi mzalendo Nyanza Road Works unaleta suluhisho la changamoto hiyo," alisema Nassoro.

Wazawa Wapata Ajira

Haji Katimba, mkaazi mwingine wa eneo hilo, amepongeza kampuni ya Nyanza Road Works kwa kutoa ajira kwa wazawa wa mtaa huo wakati wa ujenzi.

Katimba pia ameshauri ushirikiano mzuri kati ya kampuni hiyo na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na wananchi katika kujadiliana mambo ya mradi huo.

Gharama na Utekelezaji wa Mradi

Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoani Mwanza, Mhandisi Ramadhan Majaliwa, ameeleza kuwa mradi ulioanza mwezi Novemba 2024 umefikia asilimia 99 ya utekelezaji wake.



"Ujenzi wa daraja pamoja na kipande cha barabara ya njia nne umegharimu bilioni sita kutokana na fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia," alisema Mhandisi Majaliwa.

Ameongeza kuwa kazi zinazobaki ni pamoja na ukamilishaji wa mitaro, zege za waenda kwa miguu na ufungaji wa kingo za daraja.

Wito kwa Watumiaji wa Barabara

Mhandisi Ramadhan amewataka watumiaji wa barabara kulinda miundombinu hiyo na kuweka maslahi yao salama kwa kuvuka barabara kupitia juu ya daraja ili kuepuka ajali.

Mradi huu unatarajiwa kuboresha mtiririko wa magari na usalama wa wakaazi wa Mabatini huku ukiwezesha pia maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default