Jiji la Mwanza Latawaliwa na Utulivu Mkubwa

Xmation Media
By -
0


Jiji la Mwanza Latawaliwa na Utulivu Mkubwa

Na Suleiman Shagata, Mwanza

Leo, hali ya barabara jijini Mwanza imeonekana kuwa kimya na utulivu mkubwa, huku maduka yote yakiwa yamefungwa na watu wachache wakionekana kupita katikati ya jiji kuelekea maeneo mengine. Uchunguzi uliofanywa katika baadhi ya mitaa ya Kitangiri, Bwiru, Kirumba, Nera, na katikati mwa jiji umeonyesha hali hii isiyo ya kawaida, huku usafiri ukiwa mdogo sana.

Kwa mujibu wa uchunguzi, usafiri unaoendelea ni wa pikipiki na baadhi ya magari ya kibinafsi, huku vituo vya mafuta vingi vikiwa vimefungwa, hali inayotia wasiwasi endapo waendesha pikipiki wataishiwa mafuta baadaye.

Kijana mmoja wa Kirumba, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema hali hii isiyo ya kawaida inaweza kuwa hatari kwa usalama wa wananchi. “Endapo mtu akiugua na kuhitaji kwenda hospitali, hapatikani usafiri wa kumpeleka, hivyo anaweza kupoteza maisha,” alisema.

Aidha, Mariam Mussa wa Nera alieleza kuwa changamoto kama hizi zinapelekea hasara kwa taifa. “Mapato ya serikali yanapotea huku wananchi wakishindwa kununua mahitaji yao ya kila siku,” alisema.

Mathayo Francis, maarufu kama "Mzazi," anayejishughulisha na biashara ya kahawa katika eneo la Mataa, Mtaa wa Makoroboi, alisema hali ya leo si nzuri. “Kila mwaka sherehe za Uhuru hufanyika huku watu wakiwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, lakini leo hali si nzuri hata kidogo. Hakuna watu mjini,” alisema.

Francis aliongeza kuwa hofu ya wananchi inazidi kuongezeka kutokana na taarifa za maandamano yanayoratibiwa kwenye mitandao bila kufahamika ni nini hasa kilicho katika agenda ya vuguvugu hilo na ni nani kiongozi wake. Alionya kwamba serikali inapaswa kuondoa sintofahamu hii, kwani kama madai ya wananchi yana maana, yafanyiwe kazi.


“Serikali na wananchi wamalize tofauti zao, kwani endapo hali kama hii itaendelea, serikali itapataje kodi? Ulinzi huu mkubwa unaofanywa ni gharama kubwa!” alisema Francis.

Hii ni onyo kwa mamlaka na wananchi kwamba utulivu wa jiji lazima uhakikishwe, na ushirikiano kati ya serikali na wananchi ni muhimu ili kuepuka hasara na changamoto zisizohitajika.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default