NA SULEIMAN SHAGATA, MWANZA
BAADHI ya wenyeviti wa masoko mbalimbali jijini Mwanza wameomba kuwepo kwa ulinzi katika maeneo hayo kama yatakuwepo maandamano tarehe 9 mwezi Desemba ili shughuli zao zisiathiriwe hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi.
Hayo yameelezwa leo katika nyakati tofauti kwenye masoko ya mbalimbali jijini hapa wakisema huduma wanazotoa ni mhimu kwa wananchi wengi wa kawaida ambao hawana uwezo wa kununua bidhaa nyingi kwa wakati mmoja.
Mwenyekiti wa soko la Magomeni katika Kata ya Kirumba, Ramadhan Maganga aliomba siku ya Desemba 9 wawepo wanajeshi wafanye doria kwenye masoko ili shughuli zao zisiathiriwe na maandamano yanayotajwa.
Alisema anashangaa kusikia ya kuwa maandamano yaliyofanyika baada ya uchaguzi kuwa yalihusisha uporaji na uharibifu wa mali badala ya kuwa ya amani na waandamanaji kuelezea dhamira yao hivyo watu kuwaelewa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko la Milongo katika Kata hiyo, Allex Mbilingi alisema wafanyabiashara katika soko hilo hawataki maandamano kwani mahitaji ya wananchi wengi yanapatikana baada ya watu kujishughulisha kila siku.
Alisema hakuna kitu kibaya kama kukaa ndani kwani mahitaji yote wanayopata kila siku ni baada ya kutoka kwenda kufanya kazi za uzalishaji mali hivyo aliwaomba wenye nia hiyo ya kuandamana wafate utaratibu wa kisheria.
Mbilingi alisema wafanyabiashara wanafanya kazi hizo bila ya usumbufu wowote hivyo alikuwa na wasiwasi kwa nini baadhi ya watu wanaandamana wakati hakuna bughudha ya ufanyaji wa shughuli zao.
Viongozi katika soko la samaki Mwaloni walisema wao wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na hakuna wasiwasi wowote ule hivyo kuomba mambo mengine yanayoweza kujitokeza serikali itatue kwa uwezo wake.




