Ujenzi wa Daraja la Sukuma Wafikia 65%: Wananchi wa Magu na Bariadi Wajawa Furaha

Wananchi wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza na Bariadi mkoani Simiyu wameelezea furaha yao kufuatia kupiga hatua kubwa kwa ujenzi wa Daraja la Sukuma, linalotekelezwa na Kampuni ya Kizalendo ya Mumangi Construction Company Ltd, mradi ambao hadi sasa umefikia asilimia 65 ya utekelezaji.

Msimamizi wa miradi ya ujenzi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi William Sanga amesema kuwa mradi huo unakwenda vizuri kwa kiwango cha juu cha ubora na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2026.

Kwa upande wake, Mhandisi wa kampuni hiyo, Omary Msafiri alibainisha kuwa daraja hilo lenye urefu wa mita 70 na upana wa mita 11.35 limefikia hatua ya kumwaga zege, huku upande wa barabara ukiendelea kuwekewa kifusi ili kuharakisha maendeleo ya mradi.

Msafiri amesema kuwa mradi huo umetoa ajira kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi, ambapo zaidi ya watu 120 wamepata ajira za muda mrefu na mfupi, hatua ambayo imechangia kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia nyingi.

Ofisa upimaji wa kampuni hiyo, Omary Ali, amesema kuwa wanafanya jitihada kubwa kukamilisha maeneo yote muhimu kabla ya msimu wa mvua kuongezeka, kwani mvua inaweza kuathiri kasi na ubora wa ujenzi.

Ali pia ametoa rai kwa wananchi wanaoishi karibu na mradi huo kulinda miundombinu hiyo muhimu, akisema kuwa serikali imetumia fedha nyingi kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa kiwango bora kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mmoja wa wanufaika wa ajira hiyo, Zakayo Nyaga kutoka Kijiji cha Ng’haya, Kata ya Sukuma, Wilaya ya Magu, amesema kuwa kazi hiyo imemsaidia kupata kipato cha kujikimu na hata kuanzisha ufugaji wa mifugo ili kuongeza kipato chake.

Mhudumu mwingine wa mradi huo, Rehema Silvester kutoka kijiji hicho hicho, ameishukuru Kampuni ya Mumangi kwa kumpa ajira inayomwezesha kupata mkate wake wa kila siku. Ameongeza kuwa mradi huo umekuwa mkombozi mkubwa kwa wanawake na vijana wanaotafuta fursa za kujikimu.

Ujenzi wa Daraja la Sukuma unatarajiwa kuimarisha usafiri na biashara kati ya Magu na Bariadi, kupunguza umbali wa safari, na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Tukiwa Pamoja Katika Kuandika Hadithi za Maendeleo ya Jamii.