TAPHATA Yadhamiria Kushirikishwa na Wizara ya Afya Katika Mchakato wa Utengenezaji wa Dawa

Xmation Media
By -
0


Na Suleiman Shagata, Mwanza


Chama cha Wateknolojia Dawa Tanzania (TAPHATA) kimeazimia kuomba ushirikiano wa karibu na Wizara ya Afya ili kushirikishwa katika sera na mikakati ya uzalishaji wa dawa ndani na nje ya nchi.



Akizungumza katika hitimisho la kongamano la kitaifa la Wateknolojia Dawa lililofanyika jijini Mwanza, Rais wa TAPHATA, Thabit Milandu, alisema dhamira hiyo inalenga kuhakikisha wataalamu hao wanashiriki moja kwa moja katika mnyororo wa utengenezaji wa dawa na kuongeza uelewa wao kuhusu taratibu za uzalishaji.


Milandu alibainisha kuwa chama hicho pia kinakusudia kukutana na Baraza la Famasi pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili kuomba ushirikiano wa karibu katika uboreshaji wa kazi zao za kitaaluma.

Aidha, alisema moja ya maazimio muhimu ni kuongezwa kwa nafasi za ajira kwa wateknolojia dawa katika sekta ya umma na binafsi, hatua ambayo itasaidia kuongeza mchango wao katika kuboresha huduma za afya kwa watanzania wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maradhi.



Wateknolojia dawa pia wameomba mamlaka husika kuwapatia mafunzo ya juu kuhusu uzalishaji wa dawa katika mataifa yenye teknolojia ya kisasa, ili kuwawezesha kupata ujuzi mpana utakaosaidia Tanzania kujenga uwezo wa ndani wa kutengeneza dawa.

Kaatika maamuzi mengine, kongamano hilo limeazimia kuhamasisha ushiriki mkubwa wa wataalamu kila mwaka ili kukuza taaluma, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wao kazini.

Eva Peter, mteknolojia dawa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, alisema kongamano hilo limempa uelewa mpya kuhusu namna bora ya kuhudumia wagonjwa na kupambana na matumizi holela ya dawa, ambayo husababisha usugu wa dawa mwilini.

Naye Joseph Michael, mteknolojia dawa kutoka Bagamoyo, alisema amepata maarifa mapya yatakayoboresha utendaji wake wa kila siku katika kutoa huduma bora zaidi.



Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default