Na Suleiman Shagata, Misungwi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Misungwi, Elly Makala, amewataka wananchi na wafanyabiashara wanaotumia Soko la Nyashishi kufuata sheria katika ulipaji wa tozo za usafi ili kuhakikisha eneo hilo linabaki safi na kuepusha mrundikano wa uchafu.
Makala alitoa wito huo leo alipokutana na wafanyabiashara wa soko hilo kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu taratibu sahihi za utoaji na ulipaji wa tozo za kuzoa taka, kufuatia kuwepo kwa sintofahamu katika suala hilo.
Alisema kutokana na kuanza kwa msimu wa mvua, ni muhimu jitihada za haraka zichukuliwe kuhakikisha taka zinakusanywa na kuondolewa kwa wakati ili kuepusha mlipuko wa magonjwa yanayoweza kusababishwa na mazingira machafu.
Aidha, Makala aliwataka wazabuni wanaohusika na kuzoa taka pamoja na viongozi wa serikali kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za halmashauri katika kuendesha shughuli za ukusanyaji wa tozo.
“Tumeweza kufikia mwafaka mzuri kuhusu namna ya kusimamia sheria katika ukusanyaji wa tozo hizo,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ntende, Lameck Sangija, alisema elimu iliyotolewa na TAKUKURU itasaidia kuondoa migongano iliyokuwepo hapo awali kutokana na kila upande kutotambua wajibu wake.
Alisema uelewa huo mpya utasaidia kurahisisha utendaji kazi kati ya viongozi wa eneo hilo, wafanyabiashara na mzabuni, jambo litakalowezesha serikali kupata makusanyo yake kwa usahihi na bila usumbufu.




