Agnes Mambo, Tanga
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani, amesisitiza umuhimu wa jamii kufuata miongozo ya wataalamu wa lishe kuhusu ulaji sahihi wa makundi yote ya chakula, kupunguza matumizi ya mafuta na sukari, na kuhakikisha mwili unapata mlo kamili unaolinda afya ipasavyo.
Kauli hii aliitoa wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani uliofanyika viwanja vya Usagara Jijini Tanga Oktoba 11, 2025. Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya “Tuungane Pamoja Kupata Chakula Bora kwa Maisha Bora ya Baadaye”, na Balozi Dkt. Batilda amesema ni jukwaa muhimu la kujadili matumizi ya mbegu za asili katika uzalishaji wa mazao bora kwa kutumia teknolojia za kisasa za kilimo.
Akizungumzia hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula katika Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda alisema ni ya kuridhisha kutokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita. Jitihada hizo zimewezesha wakulima wengi kupata huduma bora za ugani na pembejeo za kilimo, ikiwemo ruzuku ya mbolea, mbegu, na viuatilifu.
> “Mwaka wa fedha 2024/25, wakulima 13,000 walinufaika na pembejeo za ruzuku zenye jumla ya tani 4,768. Aidha, jumla ya hekta 100,002 zililimwa na kuzalisha tani 1,814,285 za mazao mbalimbali ikiwemo mihogo, mpunga, mahindi, viazi, kunde, mbaazi na jamii nyingine za maharage,” alibainisha.
Dkt. Batilda pia aliwataka wananchi kuendelea kutunza chakula, kuongeza juhudi katika kulima mazao, na kubaini vyakula vya asili vinavyoweza kuongeza muda wa maisha na kuimarisha afya, akitoa mfano wa wananchi wa Vietnam.
Alisema:
> “Wenzetu wa Vietnam wamegundua vyakula vya asili vinavyomfanya mtu adumu miaka mingi, ikiwemo viazi mbatata na uyoga. Hivyo, ni wajibu wetu kutafakari na kushirikiana ili kulima vyakula vyetu vya asili na kuhakikisha wananchi wanavitumia kwa afya zao.”
Dkt. Batilda pia aliwashukuru wadau wa kilimo, akitoa mfano wa benki ya kilimo kwa kuanzisha mbegu za vyakula vya asili kama vile mahindi ya zambarau na njano, ambavyo vinawezesha afya bora na maisha marefu.
Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani hutoa fursa kwa jamii kutafakari nafasi ya chakula katika maisha yao, kuimarisha mifumo endelevu ya uzalishaji, na kukuza uelewa wa lishe bora. Kupitia maadhimisho haya, wananchi hukumbushwa wajibu wao wa kulinda rasilimali, kutumia vyakula vya asili kwa tija, na kushirikiana kujenga mustakabali bora wa chakula na afya nchini.

.jpg)



