Semina ya TAKUKURU Tanga: Wanahabari Wapewa Nguvu ya Kukemea Rushwa

Xmation Media
By -
0

Waandishi wa Habari Waaswa Kuendeleza Mapambano Dhidi ya Rushwa

Agnes mambo xmation media tanga




Tanga – Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewataka waandishi wa habari nchini kutumia kalamu zao kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa, ikibainisha kuwa wana nguvu ya ziada ya kufikisha taarifa muhimu zinazoweza kuelimisha na kuhamasisha wananchi.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah, ametoa wito huo wakati wa semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu nafasi yao katika kuzuia rushwa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Ndwatah amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kuhakikisha kalamu zao zinasaidia katika upatikanaji wa viongozi waadilifu, ambao hawatakuwa tayari kuona wananchi wakikosa huduma muhimu kutokana na vitendo vya rushwa vinavyohujumu miradi ya maendeleo.

“Tunapaswa kuunganisha nguvu moja. Lengo ni kuendeleza mapambano. Kila mmoja ana nafasi yake, na wanahabari wana nguvu ya ziada kutumia vyombo vyao kufikisha taarifa kwa wananchi walio wengi,” amesema Ndwatah.

Amefafanua kuwa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, wananchi wanapaswa kuelewa thamani ya kura zao na kuhakikisha hawachagui viongozi kwa misingi ya rushwa.

“Rushwa ni adui wa haki na ni kikwazo cha maendeleo. Hii ni fursa muhimu ya kutengeneza viongozi waadilifu. Pamoja na kuwa ni kosa la jinai, rushwa pia ni jambo baya katika imani zote za dini,” alisisitiza.

Aidha, amewataka waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi namna ya kuwapata viongozi bora na kuendelea kufichua vitendo vya rushwa, lakini bila kumuonea mtu, badala yake kutenda haki wakati wote.

Kwa upande wake, Jaspar Mmbaga, Afisa Mchunguzi Kiongozi Msaidizi wa TAKUKURU Tanga, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa, ambapo hatua ya kuelimisha jamii ni sehemu ya kuzuia vitendo hivyo visianze kushamiri.

Naye George Sembony, mwandishi mkongwe aliyeshiriki semina hiyo, ameshauri viongozi wa kisiasa kuonesha dhamira ya dhati katika mapambano dhidi ya rushwa ili taifa liweze kusonga mbele kwa ustawi na maendeleo.

Kwa upande mwingine, Mariam Mayaya, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, ametambua mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika mapambano dhidi ya rushwa na kusisitiza ushirikiano endelevu kati ya taasisi hiyo na vyombo vya habari.

Semina hiyo iliyofanyika mkoani Tanga imehudhuriwa na zaidi ya waandishi 50 kutoka vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii, ambapo washiriki walipatiwa elimu juu ya nafasi ya wanahabari katika kudhibiti rushwa kuelekea uchaguzi mkuu.


Tags:

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default