Na Suleiman Shagata – Mwanza
MZIKI wa sasa unatakiwa kuwa na ladha ya utamaduni wa Kitanzania ili kuendelea kutunza na kulinda utamaduni wetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, pamoja na kuhifadhi utambulisho wa Mtanzania.
Wito huo umetolewa leo Jijini Mwanza na Mwalimu Mstaafu wa Masomo ya Utamaduni, Fumbuki Lubasa, aliyesisitiza umuhimu wa wanamuziki kuandika nyimbo zao kwa kufuata misingi ya kitaaluma ya muziki, ikiwemo matumizi ya staff notation (alama za kimuziki).
Lubasa amesema kuwa kuandika nyimbo kwa alama za kimuziki husaidia kuifanya kazi ya msanii kutambulika kirahisi, kudumu kwa muda mrefu, na kulindwa dhidi ya wizi wa kazi za ubunifu. Aidha, amesema nyimbo zilizoandikwa kitaaluma huwa na mpangilio mzuri unaomwezesha msikilizaji kupata muziki wa ubora wa hali ya juu.
“Ufuataji wa namna wimbo ulivyoandikwa humfanya msanii kutambulika na kazi yake kudumu, kwani haiwezi kuibiwa kirahisi,” amesema Lubasa.
Ameongeza kuwa kwa sasa baadhi ya waimbaji wanatumia maneno ya mapenzi yasiyofaa kusikilizwa katika mazingira ya kifamilia au ya heshima, hali inayopunguza thamani ya muziki huo katika jamii.
Kwa mujibu wa Lubasa, muziki mwingi wa sasa unafanana kwa kiasi kikubwa, hali aliyoifananisha na mfumo wa copy and paste, jambo linalotokana na kutotumia misingi sahihi ya uandishi wa nyimbo kwa kutumia staff notation.
“Kutotumia misingi ya uandaaji wa muziki kunapunguza ubunifu wa wasanii,” ameongeza.
Akitoa mfano wa muziki wa zamani, Lubasa amesema nyimbo za wasanii kama Mbaraka Mwishehe, Said Mwinjuma, na Rwambo Makiadi zilikuwa na mvuto mkubwa kutokana na ujumbe mzuri, lugha ya heshima, na kufuata misingi ya kitaaluma ya muziki.
“Maneno yanayotakiwa kuongelewa chumbani leo yanaimbwa hadharani. Hebu sikiliza muziki wa zamani, ulikuwa na maadili na mvuto wa kipekee,” amesema.
Lubasa, ambaye amehitimu masomo ya utamaduni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, amewashauri wanamuziki wa sasa kujenga utamaduni wa kuandika nyimbo zao kabla ya kuziimba ili kupata sauti bora, muziki wenye ubora, na kulinda urithi wa utamaduni wa Kitanzania.
.png)

