Na Suleiman Shagata, Mwanza
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehitimisha mchakato wa kumpata Meya na Naibu Meya wa Jiji la Mwanza katika kikao kilichofanyika leo wilayani Nyamagana, ambapo aliyekuwa Meya wa Jiji hilo kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, Constantine Sima, ameibuka mshindi tena kwa kupata kura 15, na hivyo kurejea kwa awamu ya pili.
Sima ambaye ni Diwani wa Kata ya Mhandu, aliibuka mshindi dhidi ya Happiness Ibasa, Diwani wa Kata ya Nyegezi, aliyepata kura 11.
Kwa upande wa nafasi ya Naibu Meya, Diwani wa Viti Maalum kutoka Nyamagana, Anita Rwezaura, ameibuka kidedea baada ya kupata kura 14, huku wagombea wengine watatu wakipata kura 3, 6 na 6.
Awali, jumla ya madiwani 10 waliomba ridhaa ya kugombea nafasi ya Umeya kupitia CCM, lakini kamati ilipitisha majina ya madiwani wawili pekee kuendelea na hatua ya mwisho katika Baraza la Madiwani.
Akizungumza baada ya ushindi, Meya mteule Constantine Sima aliwashukuru madiwani na viongozi wa chama kwa kumuamini kwa mara ya pili, akiahidi kuendelea kutumikia wananchi kwa juhudi na uadilifu.
“Naahidi kuwatumikia wananchi kwa nguvu zote katika kuboresha miundombinu, huduma za afya na elimu,” alisema Sima.
Ameongeza kuwa kipaumbele chake cha kwanza ni kushughulikia changamoto za miundombinu na kuhakikisha barabara zote zenye ubovu zinarekebishwa ili kurahisisha huduma kwa wananchi.
Mchakato wa chama sasa umekamilika, na kesho Baraza la Madiwani linatarajiwa kuidhinisha rasmi majina hayo kabla ya viongozi hao kuanza majukumu yao, sambamba na uapisho wa madiwani wote katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

